1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Karibu familia 2,500 zapoteza makaazi Marsabit

26 Agosti 2022

Jumla ya familia 2,500 kutoka eneo bunge la Saku katika jimbo la Marsabit zimepoteza makaazi yao baada ya kuzuka kwa machafuko ya kikabila eneo hilo kati ya mwaka 2018 na 2021.

Afrika Nahrungsmittelspende Church World Service Organisation in Marsabit
Picha: Michael Kwena/DW

Ripoti iliyotolewa na Mamlaka ya Kukabili Majanga, NDMA, jimboni humo aidha imeonyesha kuwa takriban nyumba 1,026 ziliteketezwa kwa moto wakati wa machafuko hayo. Na kama anavyoeleza Michael Kwena kutoka Marsabit, 

Kwa miaka minne tangu kuzuka kwa machafuko ya kikabila yaliyopelekea mamia ya watu kufariki katika kaunti hii, familia kadhaa bado hazijarejea makwao kwa kuhofia kushambuliwa. Ripoti iliyotolewa na NDMA iliyochunguza hasara iliyotokana na machafuko hayo, imebainisha kuwa takriban watu elfu kumi na tano walikimbia na kugeuka kuwa wakimbizi wa ndani katika jimbo hili.

Baadhi ya viongozi kutoka hapa Marsabit, sasa wanaitaka serikali ya kaunti kwa ushirikiano ya ile ya kitaifa kuwarejesha makwao wakimbizi hao wa ndani kama sehemu ya kurejesha utulivu katika maeneo yaliyoathirika na machafuko hayo. Chachu Ganya na mbunge anayeondoka wa Horr Kaskazini: "Tuna tatizo la amani kwenye hii kaunti. Leo kuna watu ambao wamekuwa wakimbizi wa ndani kati yao. Hakikisha watu waliofurushwa makwao wanarejeshwa makwao…"

Viongozi wa Marsabit wanataka serikali iwarejeshe watu makwaoPicha: Michael Kwena/DW

Kulingana na mwakilishi mteule wa Marsabit ya Kati, Jack Elisha Godana, jimbo la Marsabit limekumbwa na changamoto kadhaa na hivyo kuna haja ya viongozi kushirikiana ili kupata suluhu kwa mahangaiko ya wakaazi. Akiongea kwenye hafla ya kumuapisha gavana wa jimbo hili katika uwanja wa michezo wa Marsabit, Godana amesema kuwa idadi kubwa ya wakaazi wanahangaika kutokana na ukosefu wa usalama jimboni hapa: "Mji huu wa Marsabit una changamoto nyingi sana na matatizo haya yatasuluhishwa na sisi viongozi. Kuna zaidi ya nyumba 300 zilizobomolewa na vijana pia wahahitaji kazi. Tafadhali, watafute viongozi wote ili tukae pamoja…"

Serikali kwa upande wake,imesema kuwa itashirikiana na viongozi wote kutafuta suluhisho la kudumu kwenye matatizo ya ukosefu wa usalama na amani ambao umeshuhudiwa hapa Marsabit kwa muda mrefu. Kamishna Paul Rotich akikariri kujitolea kwa idara ya usalama katika kuwahudumia wakaazi wote wa kaunti hii: "Hatuwezi kupata matunda ya amani iwapo hatutakuwa na usalama wa kudumu. Tuko tayari kuwashika mkono ili kuhakikishia tunatoa huduma katika kila pembe ya kaunti."

Kaunti ya Marsabit imeendelea kukumbwa na matatizo kadhaa ikiwemo suala la ukame hali ambayo imechangia idadi kubwa ya wakaazi kuhitaji chakula cha msaada. Mbunge mteule wa Laisamis, Joseph Lekuton, akimtaka gavana Mohammud Ali kuomba msaada kutoka kwa mashirika ya kimataifa ili kuwasaidia maelfu ya wakaazi wanaokabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na hali mbaya ya ukame unaoshuhudiwa wakati huu.

"Tuna shida ya njaa na watu wanaumia na pia mifugo wanakufa. Tunataka uombe msaada kutoka mashirika ya kimatifa ili tuwasaidie watu wetu”

Mwezi Mei mwaka huu, serikali iliagiza kuendeshwa kwa oparesheni ya polisi iliyolenga kutwaa bunduki haramu kutoka mikononi mwa raia kama sehemu ya kuthibiti machafuko katika jimbo hili.

Mwandishi: Michael Kwena/DW Marsabit

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW