1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Kina mama watoa wito 'mogoka' ipigwe marufuku pwani

Eric Ponda24 Agosti 2018

Kina mama katika pwani ya Kenya wanataka serikali kupiga marufuku uuzaji na utafunaji wa majani ya miraa maarufu kama 'mogoka' wakisema unawafanya vijana wengi kujiingiza katika uraibu huo mbaya huku wakiachana na masomo

Jemen Volksdroge Khat Mann mit Blättern
Picha: picture-alliance/dpa/Y. Arhab

Katika ukanda wa Pwani nchini Kenya, makundi ya kina mama yanaitaka serikali kupiga marufuku uuzaji na utafunaji wa mmea wa miraa katika ukanda huo, wakisema kuwa uraibu huo umechangia pakubwa kuzorota kwa maadili miongoni mwa jamii.

Makundi hayo ya kina mama kutoka jimbo la Kilifi na Mombasa, wanasema kuwa biashara ya majani ya miraa yanauzwa rejareja katika soko la wazi kwa bei ya chini na hivyo kuwaingiza vijana wengi katika uraibu huo..

Mogoka ni majani mabichi yanayotokana na zao la miraa ambalo ni maarufu sana kote ulimwenguni kutokana na kileo chake. Majani haya yanadaiwa kuwa na ulevi mkali zaidi hata kushinda utafunaji wa kawaida wa miraa.

Kwa wanaotumia majani haya, wanasema kuwa ulevi wake ni maradufu na hutafunwa yakiwa mabichi kinyume na miraa ambayo watu hutafuna vijiti vyame.

Makundi hayo ya kina mama yaliyojipa jina maarufu kama Kilifi Mums na Mombasa Mums, yanasema kuwa watoto wengi wa ukanda wa Pwani hawazingatii tena masomo.

Mogoka ni majani mabichi yanayotokana na zao la miraa ambalo ni maarufu sana kote ulimwenguni kutokana na kileo chake. Majani haya yanadaiwa kuwa na ulevi mkali zaidiPicha: DW/R.Krause

Ndoa zavunjika

Makundi hayo ya kina Mama yanasema kuwa ndoa nyingi katika ukanda wa Pwani pia zimevunjika huku visa vya ujambazi na utovu wa usalama vikiongezeka ndani ya majimbo hayo mawili

Makundi hayo ya kina mama yaliandamana kuilalamikia serikali kuchukua hatua za haraka kupiga marufuku uingizwaji wa bidhaa hiyo ndani ya Ukanda wa Pwani.

Kiwango cha elimu katika majimbo haya mawili kimekuwa kikishuka huku watoto wengi wa kike wakipata mimba za mapema.

Kwa kawaida zao hili ambalo hukuzwa kwa wingi katika bara Mwa Kenya hususan maeneo la Mlima Kenya, Jimbo la Meru, ni biashara kubwa iliyokita mizizi mkoani Pwani.

Makundi hayo yanadai kuwa uraibu huu ni sawa na watu wanaotumia dawa za kulevya ambavo zimewadumaza vijana wengi wa ukanda wa Pwani.

Afisa wa masuala ya watoto jimo la Kilifi Kennedy Owino anasema kuwa idara yake inafuatilia kwa makini suala hilo baada ya kufaulu kupiga marufuku densi za kesha ambazo zilichukua nafasi ya kwanza katika mimba za mapema miongoni mwa wasichana wadogo wa shule.

Juhudi za Dw kutaka kauli ya serikali kuhusiana na hoja hii hazikufaulu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW