Kenya kuchoma tani za pembe za ndovu na faru
30 Aprili 2016Kenya itachoma tani 105 za pembe za ndovu na zaidi ya tani moja ya pembe za faru leo Jumamosi (30.04.2016) ikiwa sehemu ya kupambana na majangili.
Leonardo DiCaprio na Elton John ni miongoni mwa watu mashuhuri watakaoshuhudia lundo la pembe za ndovu likichomwa moto wakati wa tukio hilo la kwanza la aina yake tangu mwaka 1989.
Kwa mujibu wa wakfu wa wanyama pori barani Afrika AWF, kiasi cha pembe za ndovu 35,000 wameuwawa katika bara la Afrika mwaka jana, kutoka jumla ya tembo 500,000.
Hali ni mbaya zaidi kwa faru. Tangu mwaka 1960, karibu asilimia 98 ya faru weusi wa Afrika, wameuwawa.
Biashara haramu
Kilo moja ya pembe ya ndovu inaripotiwa na shirika linalopigania ulinzi wa wanyamapori kuwa ina thamani ya dola 1,100 katika soko la chini kwa chini, wakati pembe ya faru inakwenda mara 50 zaidi ya kiasi hicho, na China ikiwa ndio soko kuu.
Mashirika ya ulinzi wa mazingira yameeleza kuunga kwao mkono kuharibiwa kwa shehena hiyo. "Kuhifadhi pembe hizo zilizokamatwa ni kazi kubwa na yenye gharama kubwa," amesema Daniela Freyer kutoka shirika la Pro Wildlife.
Pia kuna hatari, wakati mataifa masikini yanaweza kupata fedha nyingi kwa kujiingiza katika biashara haramu ya pembe za ndovu.
Serikali ya Kenya kwa muda mrefu ilikuwa inataka kupigwa marufuku biashara hiyo duniani, wazo litakalojadiliwa tena katika mkutano wa shirika la CITES ambao unaanza mjini Johannesburg mwishoni mwa mwezi Septemba.
Nchi nyingi zimepiga marufuku biashara ya pembe za ndovu katika miaka ya 1980, lakini kuna tofauti, wakati China na Japan zinaruhusu kununua pembe hizo kutokana na kulegezwa kwa vizuwizi, Freyer amesema.
Wanastahili maisha zaidi
Mamlaka ya hifadhi ya mali asili nchini Kenya imelitangaza tukio la leo Jumamosi katika ukurasa wa Twitter chini ya hashtag: "worthmorealive" wanastahili maisha zaidi.
Dai hilo hakika ni la kweli kwa ajili ya nchi hiyo ya Afrika mashariki ambayo ni maarufu kwa utalii, ambayo imejipatia kiasi ya dola bilioni 2.2 ama kiasi ya asilimia 4 ya pato jumla la taifa kutokana na utalii mwaka jana, kwa mujibu wa shirika la utalii la dunia.
Zaidi ya asilimia 9 ya wakaazi milioni 46 nchini Kenya wanafanyakazi katika sekta hiyo, wakati idadi inaongezeka kila mwaka. Watalii wanavitiwa nchini humo na maili kadhaa za fukwe nzuri katika bahari ya Hindi na mbuga za wanyama ndani ya nchi hiyo.
Gavin Shire kutoka kitengo cha samaki na wanyamapori nchini Marekani FWS amesema kwamba maafisa wa Kenya wanahitajika kuhakikisha kwamba pembe hizo zinaharibiwa katika njia ambayo inafanya soko haramu la pembe hizo linakuwa halifai.
Mwandishi. Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Yusra Buwayhid