Kenya kuendesha oparesheni kusaka majangili
15 Machi 2023Mashambulizi na mauaji katika maeneo hayo bado yanaendelea licha ya oparesheni ya kiusalama inayofanyika katika kaunti 6 zilizoainishwa kuwa hatari.
Sammy Yatich aliamkia taarifa za mwanamme mmoja kuwawa na mifugo zaidi ya 200 kuibwa eneo anokoishi Baringo Kaskazini.
Majangili hao pia walitekeleza uvamizi mwingine mchana wa leo katika eneo la Baringo Kusini.
Soma pia:Serikali yawatafutia maji wafugaji Kenya
Mapema wiki hii Waziri wa usalama wa ndani Kithure Kindiki alitangaza masaa 24 kwa watu wanaoishi kwenye milima na mapango 27 katika kaunti 6 zilizoainishwa kama hatari kuyahama makaazi yao.
Hatua hii imechukuliwa na serikali ili kuwapa nafasi ya kukabiliana vilivyo na majangili wanaoaminika kutumia mapango na milima hiyo kama maficho yao.
"Atakayepatikana katika maeneo hayo kuanzia jumatatu saa mbili wiki hii, atachukuliwa kuwa mshukiwa wa ujangili.” Alisema waziri wa usalama Kenya
Muda huo uliotolewa umekamilika, na taswira katika maeneo haya ni ya magari ya kijeshi yakikokota mizinga na zana za kivita za kukabiliana na magaidi, yakielekea maeneo ya oparesheni.
Shule zafungwa kupisha oparesheni
Shule nyingi katika maeneo haya zimeanza likizo fupi mapema ili waalimu na wanafunzi wasije wakapatikana hapa wakati wa oparesheni.
Lakini licha ya agizo hilo la serikali, wezi wa mifugo wameendelea kuwavamia na kuwaua watu wasiokuwa na hatia.
Wakaazi wanapinga amri ya serikali ya kuwahamishawakisema inayavuruga maisha yao.
Wengi hawajui pa kwenda na wanahofu iwapo wanakokwenda kuna usalama au watakutana na mauti yao.
Soma pia:Uamuzi wa Mahakama ya juu wawapa hofu viongozi wa dini Kenya
Akizungumza na kituo kimoja cha habari hii leo, Mbunge wa Kacheliba Titus Lotee ameikosoa serikali kwa kuiadhibu jamii nzima badala ya kuwaendea wahalifu.
"Kama Waziri anasema kwamba anataarifa kamili kuhusu watu wanaochochea uhalifu huu, kwa nini aadhibu jamii zote?"
Alihoji mwanasiasa huyo anaewakilisha eneo hilo katika bunge.
Oparesheni hii sasa inaongozwa na naibu mkuu wa polisi nchini Noor Gabow.