1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kufunga Dadaab baada ya miezi sita

16 Novemba 2016

Serikali ya Kenya imesema kwamba imeamua kuchelewesha kufungwa kwa kambi ya wakimbizi ya Dadaab ambayo inaichukulia kuwa tishio la usalama, baada ya shinikizo la kimataifa la kutaka kuwapa wakimbizi hao muda zaidi

Flüchtlingslager Dadaab Kenia
Picha: AP

Waziri wa mambo ya ndani wa Kenya Joseph Nkaissery amesema kwamba serikali imeamua kuongeza muda wa kufunga kambi hiyo ya Dadaab iliyo makazi ya takriban wakimbizi wa kisomali elfu 280 kwa miezi sita zaidi .
Nkaissery amesema kuwa serikali hiyo imeongeza muda huo baada ya shirika la umoja wa mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR kuomba kuongezwa kwa muda huo. Alikanusha madai ya Kenya kuwalazimisha wakimbizi hao kurejea nchini Somalia inayokumbwa na ghasia .
Hatua hiyo ya Kenya ya kutaka kufunga kambi hiyo ni kutokana na madai ya nchi hiyo kwamba kambi hiyo inatumiwa na wanamgambo wa kiislamu kutoka nchi jirani ya Somalia ambao wamefanya msururu wa mashambulizi nchini humo. 
Lakini makundi ya kutetea haki za binadamu yamekosoa uamuzi huo na kusema itawaumiza wakimbizi hao waliotoroka vita na umaskini. 

Serikali haipingi uhamiaji wa hiari
Nkaissery alisema, "serikali imekubali ombi la kuongeza muda wa kuwahamisha wakimbizi hao wa kisomali na hatua hii ni muhimu kuwezesha kufungwa kwa kambi hiyo baada ya miezi sita." 
Ameuambia mkutano wa waandishi wa habari  kuwa hatua ya hiari ya kurejea nyumbani kwa wakimbizi hao itaendelea bila pingamizi.
Wiki hii, afisa mkuu wa wizara hio aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba muda wa mwisho wa  mwezi Novemba hautaheshimiwa ijapokuwa hakutoa mweleko mpya. Afisa huyo alisema kuwa kambi hiyo sasa ni makazi kwa takriban watu elfu 250 huku maafisa wa umoja wa mataifa wakisema kuwa idadi hiyo ilikuwa elfu 350 mwanzoni mwa mwaka huu. 
Takriban watu nusu milioni waliishi katika kambi hiyo miaka michache iliyopita.
Kulingana na Gerry Simpson mtafiti mkuu wa maswala ya wakimbizi wa kundi moja la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini New york, "Kenya inapaswa kufutilia mbali vitisho vyake vya kufunga kambi ya Dadaab . Shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia maswala ya wakimbizi pamoja na wahisani wanapaswa kuishinikiza Kenya kuwahakikishia hadharani wakimbizi hao kwamba wanakaribishwa nchini humo wakati wowote hadi pale itakapokuwa salama kwao kurejea nchini mwao," amesema mtafiti huyo.

Wakimbizi katika kambi ya DadaabPicha: WFP/Rose Ogola7/picture alliance/dpa

Kenya yalaumiwa
Shirika la Amnesty International na wakimbizi waliorejea nchini Somalia , walisema kuwa maafisa nchini Kenya wanawalazimisha wakimbizi hao kurejea Somalia ambapo wanakabiliwa na hatari ya kuuawa ama kujumuishwa kwa lazima katika kundi la wanamgambo la al-Shaabab.
Baadhi ya wakimbizi waliorejea nchini Somalia waliliambia shirika la habari la Associated Press kuwa kwasasa wanakabiliwa na njaa licha ya ahadi zilizotolewa kwamba watapata usaidizi. 
Serikali ya Somalia inayoungwa mkono na mataifa ya Magharibi inakabiliwa na tatizo la ugaidi katika juhudi zake za kujiimarisha baada ya vita ya miaka mingi.
Maeneo mengi ya nchi hiyo hayana huduma za kimsingi.


Mwandishi:Tatu Karema/ Reuters/AP
Mhariri: Gakuba Daniel

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW