1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kuongoza vita dhidi ya ugaidi Afrika Mashariki

26 Februari 2024

Mikakati ya kupambana na ugaidi na vitisho imepata msukumo mpya baada ya wadau kukutana nchini Kenya kuimarisha mbinu za muda mrefu za kuzuwia na kupambana na ugaidi pamoja na misimamo mikali ya kidini.

Somalia al-Shabaab
Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Somalia ambalo hufanya mashambulizi yake pia nchini Kenya.Picha: picture alliance / AP Photo

Kenya iliyojiunga na Shirika la Kimataifa la Uangalizi na Utafiti wa Vitisho vya Kigaidi (GCTF) mwaka 2023 ilisema inapania kuongoza tawi la Afrika Mashariki kwa ushirikiano na Kuwait, licha ya kurejeshwa tena kwenye orodha ya mataifa yaliyo na mbinu dhaifu za kupambana na utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi.

Kwenye taarifa yake, Mkurugenzi wa Kituo cha Kupambana na Ugaidi nchini Kenya, (NCTC), Rosalind Nyawira, alibainisha kuwa lengo lao ni kuleta uwiano na kubadilishana mawazo kwenye suala zima la kupambana na ugaidi kwa kuzingatia pia usajili wake na kuwawezesha raia wa nchi husika kuupiga vita uhalifu huo.

Soma zaidi: Kenya yaonya juu ya kitisho cha mashambulizi ya kigaidi

Akiwa eneo la kaskazini mashariki mwa nchi, Spika wa Bunge la Kenya, Moses Wetangula, aliusisitizia umuhimu wa kulinda amani na kuupiga vita ugaidi kwa kutilia maanani kitisho cha kundi la al- Shabaab la Somalia.

Matumizi mabaya ya sheria za ugaidi Afrika Mashariki

This browser does not support the audio element.

“Na hapa Garissa, hapa Bura, tukielekea baharini tuna changamoto kubwa ya usalama. Na lazima tuendelee, hata tukiwa na vijana wetu wa jeshi, hatuna budi kushirikiana na serikali ili tuwatoe wale watu wabaya katika jamii." Alisema spika huyo.

Ushirikiano wa Kenya na Kuwait

Kenya na Kuwait ziinataka kutimiza azma ya kuchukuwa uwenyekiti wa Shirika la GCTF Kanda ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Nyawira, Kenya na Ujerumani zimependekeza kuongoza mpango unaojikita katika uhusiano kati ya athari za mabadiliko ya tabianchi na ugaidi.

Mkutano huo ulioandaliwa na Umoja wa Ulaya pia ulilenga kuangazia operesheni za uangalizi wa vitendo vya ugaidi kwa jicho la kikanda.

Soma zaidi: Kenya: Waathirika wa mashambulizi ya ubalozi wa Marekani bado kufidiwa

"Kenya na Umoja wa Ulaya kwa pamoja zinataka kuyashirikisha mashirika ya jamii ili kubadili mitazamo na juhudi za kurejea kwenye maisha ya kawaida." Alisema Ondrej Simek, naibu balozi wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Kenya.

Kikao hicho cha pembeni kitajadili pia ufadhili wa shughuli za kigaidi za kundi la al-Shabaab, mchango wa misimamo mikali ya kidini na pia mifumo bora ya kuzuwia ugaidi kwa jumla.

Miaka 25 tangu mashambulizi ya kigaidi Nairobi na Dar

03:33

This browser does not support the video element.

"Kwa mara nyengine aya (kitabu cha Qur'an) zinabadilishwa kwa njia isiyokuwa mwafaka ambapo kwamba watu wanaweza wakafikiria kwamba Uislamu ni ugaidi. Kwa mfano neno 'jihadi' lililo na maana nyingi tofauti. Jambo la pili ni kwamba kuwa na uwiano na kuangazia shida mbalimbali zilizoko katika jamii ili kuweza kupambana na ugaidi ana kwa ana." Alisema Abdikadir Adam Juma ni mwakilishi wa Chama cha Waislamu wa Kenya katika Kaunti ya Nakuru

Majadiliano hayo yatatumika kuandaa mambo ya msingi yatakayopewa kipaumbele na tawi la Afrika Mashariki.

Kenya yarejeshwa orodha ya wenye mifumo dhaifu

Wakati huo huo, Kenya imerejeshwa tena kwenye orodha ya mataifa 23 yaliyo na mifumo dhaifu ya kupambana na utakatishaji wa fedha, ugaidi na ulanguzi wa mihadarati.

Matokeo ya mashambulizi ya kundi la kigaidi la Somalia, al-Shabaab, mjini Mogadishu.Picha: Mariel Müller/DW

Kwenye kongamano linaloendelea mjini Mombasa la kupambana na mihadarati, Waziri wa Masuala ya Jinsia, Utamaduni na Sanaa Aisha Jumwa alisisitiza kuwa serikali iko imara kwenye vita hivyo.

Soma zaidi: Marekani yafanya kumbukumbu ya mashambulizi ya Nairobi, Dar

"Kwa hivyo, kila mtu anapiga vita mihadarati. Si haki na hatutaki tufanye maandamano. Hawa jamaa zako hawa wafanye kazi vilivyo." Alisema waziri huyo.

Kwa upande wa mataifa ya Afrika Mashariki, Uganda imefanikiwa kuondolewa kwenye orodha hiyo, lakini Tanzania na Sudan Kusini bado zimeendelea kusalia.

Mataifa mengine ya Afrika kwenye orodha hiyo ni Nigeria, Afrika Kusini, Mali, Msumbiji, Burkina Faso, Senegal na Kameruni.

Hatua hii ina maana kuwa Kenya iliyo na ushawishi mkubwa kifedha kwenye soko la Afrika Mashariki itatazamwa kwa jicho la karibu zaidi kwenye masuala ya kusaka mikopo ya kimataifa na pia hadhi yake.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW