1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kushirikiana na Israel kiteknolojia katika kilimo

10 Novemba 2022

Wakati huu ambapo mataifa mengi ya pembe ya Afrika ikiwemo Kenya yanakabiliwa na ukame, serikali ya Kenya inafikiria namna inavyoweza kuimarisha uzalishaji wa chakula.

Eco Africa - Die Drohnen-Technologie bringt die Landwirtschaft in die Zukunft
Picha: DW

Serikali hiyo imefanya mkataba na taifa la Israeli utakaoiwezesha nchi hiyo kuboresha kilimo kupitia teknolojia ya kisasa pamoja na kupanua soko la mazao yake. 

Kenya inalenga kuvutia uwekezaji zaidi kwenye sekta ya kilimo katika juhudi za kupambana na upungufu wa chakula cha kutosha nchini humu.

Kongamano la serikali kuhusu kilimo nchini Kenya

Ni kwa mwelekeo huo kwamba ziara ya balozi wa taifa la Israeli mjini Nakuru imeangazia ushurikiano kati ya nchi hizi mbili kwenye teknolojia ya uzalishaji wa mbegu, kilimo cha umwagiliaji ili kupambana na mabadiliko ya tabia nchi yanayoshuhudiwa nchini.

Teknolojia hiyo pia inanuiwa kumuwezesha mkulima kufahamu zaidi namna ya kujitayarisha kwa mabadiliko haya.

Balozi wa Israel nchini Kenya Michael Lotem amehimiza umuhimu wa kujumuisha sekta ya kibinafsi kwenye juhudi hizi, ili kuweza kufaidi kutokana na utaalam uliopo.

Kenya ni miongoni mwa nchi zinazoathiriwa na ukame miongoni mwa nyingine katika pembe ya Afrika.Picha: Dong Jianghui/Xinhua/picture alliance

Eneo la bonde la ufa limetambulika kwa muda mrefu kama kapu la chakula na limekuwa tegemeo la wengi nchini Kenya.

Lakini kinyume na desturi hii, eneo hili lilijumuishwa pamoja na kaunti 29 zilizo kwenye orodha ya kaunti zilizoathiriwa na ukame na baa la njaa, kaunti 10 zikiwa kwenye hali mbaya zaidi.

Akiongoza zoezi la usambazaji wa chakula cha msaada kutoka kwa serikali, Gavana wa kaunti ya Nakuru Susan Kihika amehimiza hitaji la kurejesha uwezo wa eneo hilo kukidhi kilimo chake.

Pamoja na kutathmini jinsi gani Kenya inavyoweza kujifunza kutoka kwa taifa la Israel, ushirikiano baina ya nchi hizi mbili unatoa fursa ya soko la kimataifa.

Balozi huyo wa Israel ameeleza kwamba eneo hili litanufaika kutokana na soko la mazao yake nchini Israel kwa bei nzuri.

Mwandishi: Wakio Mbogho/DW, Nakuru.