Kenya kutengeneza vidonge vya kumeza kupambana na COVID 19
3 Machi 2022Kampuni ya Universal Corporation iliyoko karibu na mji wa Kikuyu nje kidogo ya Nairobi itavitengeza vidonge hivyo vya kupambana na COVID 19 ikiwa ni mara ya kwanza dawa ya aina hii kutengenezwa.Wamiliki wa kampuni ya Universal inayotambuliwa na shirika la Afya ulimwenguni, WHO, ni Strides Pharma Science ya India ambayo pia inatengeza dawa za kupambana na makali ya Ukimwi, ARV.
Molnupiravir ni dawa ya kwanza ya kumeza iliyopata ridhaa ya kupambana na COVID 19.Dr Willis Akhwale ni mwenyekiti wa jopokazi la kupambana na COVID 19 nchini Kenya na huu ndio mtazamo wake.
Mkataba huo ulifikiwa kati ya kampuni ya utafiti na bidhaa utabibu ya Merck iliyo na kibali kamili pamoja na shirika la Medicines Patent Pool linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa kuzishusha bei za dawa kwa mataifa masikini. MPP ni shirika linalojihusisha kwa karibu kuzipinguza bei za dawa za kupambana na makali ya Ukimwi, Hepatitis yaani homa ya ini na Kifua Kikuu.
Walio chini ya miaka 18 hawapaswi kutumia dawa hizo
Shirika hilo liliteua kampuni 27 katika mataifa ya Bangladesh, China, Misri,Jordan, India, Indonesia, Pakistan, Afrika Kusini, Korea Kusini, Vietnam na Kenya. Molnupiravir ni dawa inayokinza au kuua virusi na iliundwa mahsusi kwa mafua.Ni dawa ya kunywa na inaweza kutumiwa nyumbani kutibu COVID 19 isiyokuwa kali. Kulingana na wataalam dawa hiyo inapaswa kutumiwa katika hatua za mwanzo za maambukizi kuepusha madhara zaidi.
Hata hivyo wagonjwa walio na umri wa chini ya miaka 18 hawapaswi kutumia Molnupiravir kwani inaweza kuathiri ukuaji wa mifupa na gegedu. Dozi yake ni vidonge 4 vya gramu 200 vinavyonywewa kila baada ya saa 12 kwa muda wa siku 5. Wakati huohuo, wizara ya afya imekanusha taarifa inayodai kuwa serikali imebadili na kulegeza sheria za kutotangamana za kupambana na COVID 19.
Taarifa hizo zilizagaa mitandaoni na wizara inashikilia kuwa hakuna kilichobadilika. Mutahi Kagwe ni Waziri wa afya na anausisitizia umuhimu wa chanjo ya COVID 19.
Kulingana na shirika la MPP la kushusha bei za dawa kwa mataifa masikini, kampuni 5 zitajikita kwenye kuandaa mali ghafi,13 zitaitengeza mali ghafi na dawa na 9 zilizosalia zitakamilisha mchakato wa kuiunda dawa.Kampuni ya Kenya iliyoteuliwa ya Universal Corporation itahusika na hatua ya mwisho za kuandaa dawa.
Mwandishi: Thelma Mwadzaya