1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kuwapa fidia waathirika wa mabadiliko ya tabianchi

Wakio Mbogho18 Septemba 2023

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, kwa mwaka huu wa 2023 pekee, Kenya imewasilisha kesi mbili kati ya 2,180 kuhusu athari ya mabadiliko ya tabia nchi.

Kenya itaanza mchakato wa kuwafidia wahanga wa mabadiliko ya tabianchi kwa awamu kuanzia Oktoba mwaka huu
Kenya itaanza mchakato wa kuwafidia wahanga wa mabadiliko ya tabianchi kwa awamu kuanzia Oktoba mwaka huuPicha: DW

Baada ya miaka mingi ya subira na makabiliano ya athari za ongezeko la maji katika Maziwa Baringo, Naivasha na Nakuru, hali iliyowafanya wakimbizi wa mabadiliko ya tabianchi na kuwaletea maafa makubwa, wakaazi wa maeneo haya huenda wakapata ahueni baada ya serikali ya Kenya kuahidi kuwafidia. Katibu msimamizi wa wizara ya mazingira ya Kenya, Festus Ng'eno, amesema mchakato huo umeanza na kaunti ya Baringo itakuwa ya kwanza kupokea fedha kutoka serikali ya Kenya na wahisani wa kimataifa.

"Baringo itakuwa kati ya kaunti za kwanza zitakazopokea fedha kutoka Umoja wa Ulaya, awamu ya pili itakuja Nakuru na Naivasha ambao ni kati ya walio kwenye mpango huo. Serikali ya kaunti inazingatia kuzisaidia jamii hizi. tunatarajia kufikia mwezi Oktoba hadi Disemba, tutakuwa tumekamilisha mkataba huo wa ufadhili.”, alisema Ng'eno.

Mchakato wa fidia 

Kenya ni miongoni mwa nchi zilizoathirika pakubwa na mabadiliko ya tabia nchiPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya UN Global Climate Litigation Report: 2023 Status Review, Kenya imewasilisha kesi mbili kati ya kesi 2,180 zilizowasilishwa kwenye hifadhi data ya madai ya hali ya hewa duniani. Moja ya kesi hizo imewasilishwa na Kituo cha Sheria ambalo ni shirika la kiraia la kutetea haki za binadamu, pamoja na jamii za Ilchamus na Tugen wanaoishi karibu na Ziwa Baringo. Wanaishtaki serikali ya Kenya kwa athari za mafuriko ya Ziwa Baringo. Ongezeko la maji kwenye maziwa maeneo haya yamewaacha raia bila makaazi, mashamba na kusababisha maafa.

Kesi ya pili ina tathmini ufafanuzi wa iwapo mamalaka ya usimamizi wa mazingira nchini, NEMA, ilikiuka masharti ya kuushirikisha umma kwenye maamuzi kabla ya kutoa leseni ya kujengwa kwa kiwanda cha mkaa mjini Lamu, ambacho kimeibua wasiwasi wa kimazingira.

Kupambana na mabadiliko ya tabia nchi

Katibu msimamizi wa wizara ya mazingira ya Kenya amesema wataanza na Baringo na baadaye Naivasha, Nakuru, Tana River na mengine. Rais Wiiliam Ruto ametoa shilingi bilioni 7.3 kwa mipango ya kaunti nchini inayolenga kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na kwasababu hiyo, katibu huyo amesema wanafanya kazi kwa ukaribu na serikali za kaunti ili kuikabili hali hasa wakati huu ambapo kuna tahadhari ya mvua kali ya El Nino ambayo huenda ikasababisha majanga.

Mataifa yamekuwa yakikutan kila mwaka kujadili uthibitisho wa makubaliano ya Paris ya mwaka 2016 ambapo mataifa yalioendelea yalijitolea kutoa dola bilioni 100 kila mwaka kuyasaidia mataifa yanayoendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ay tabia nchi.