1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Maafisa wa uchaguzi wakesha wakihesabu kura

Sylvia Mwehozi
10 Agosti 2022

Zoezi la kuhesabu kura katika uchaguzi mkuu wa rais uliofanyika jana nchini Kenya, limeendelea usiku kucha wa kuamkia Jumatano huku Wakenya wakisubiri kwa hamu matokeo rasmi.

Kenia Wahlen 2022
Picha: Luis Tato/AFP

Ushindani mkubwa katika kinyang'anyiro cha urais ni baina ya wagombea wawili, naibu wa rais William Ruto na mwanasiasa mkongwe Raila Odinga.

Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC inakabiliwa na shinikizo la kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki. IEBC imekiri kwamba takribani vifaa 200 vya kielektroniki vya kuwatambua wapiga kura vilishindwa kufanya kazi kati ya vifaa 46,000.

Wananchi wengi wa Kenya wana matumaini na kura ya mwaka huu kuwa italeta mabadiliko katika maisha ya kila siku wakati wakikabiliwa na kupanda kwa gharama za maisha na mfumuko wa bei.

Umati wa wapiga kura waliojitokeza kupiga kuraPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Saa moja kabla ya vituo vya kupigia kura kufungwa, idadi ya waliojitokeza kushiriki uchaguzi ilikuwa ni asilimia 56 ya wapiga kura walijiandikisha. Vituo vya kupigia kura vimefungwa Kenya baada ya uchaguzi uliodumu kutwa nzima. Jumla ya wapiga kura milioni 22.1 waliandikishwa kushiriki kwenye zoezi la kihistoria.

Usalama umeimarishwa kwenye ukumbi wa Bomas wa Kenya ambacho ndicho kituo rasmi cha kukusanya na kujumlisha matokeo ya uchaguzi. Mshindi wa kinyang'anyiro cha urais atatangazwa kutokea Bomas.

Wagombea wakuu wa uchaguzi wa urais Kenya wapiga kuraLicha ya kampeni chafu zilizogubikwa na maneno ya kupakana matope na madai ya udanganyifu, utulivu umeshuhudiwa kwa kiasi kikubwa wakati wa kura ya jana ikiwemo Kisumu na Eldoret, Maeneo haya yalishuhudia ghasia mbaya za baada ya uchaguzi mwaka 2007. Joyce Kosgei kutoka kijiji cha Kosachei ambako Ruto alipigia kura anautizama uchaguzi wa jana kuwa wa tofauti na wa kipindi cha nyuma, akisema ulikuwa wa utulivu na amani.

Awali tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC ilikuwa tayari imeahirisha chaguzi kadhaa ikiwemo kura za ugavana katika mji wa bandari wa Mombasa. IEBC ilitaja hitilafu katika karatasi za kupigia kura kama sababu za kuahirisha kura. Lakini kwa ujumla, uchaguzi umemalizika salama katika maeneo mengi, huku wapiga kura vijana na watu wazima wakijitokeza kuleta mabadiliko.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW