Kenya: maandamano yarejea tena kudai uwajibikaji
16 Julai 2024Hali ni ya wasiwasi katikati ya jiji la Nairobi ambako maduka yamefungwa na idadi ya watu wanaotembea sio ya kawaida. Polisi wanapiga doria na baadhi ya barabara zimefungwa. Polisi wamefyatua makopo ya gesi ya kutoa machozi ili kuwatawanya waliokuwa wanakusanyika. Moshi ulihanikiza na baadhi wanaonekana wakiosha nyuso zao. Pikipiki kadhaa zimetelekezwa wakati wa mshike mshike huo.
Polisi waliojihami wanaonekana nje ya afisi muhimu za serikali kama Ikulu ya Nairobi, bunge la Taifa na mahakama ya juu. Dhamira ya maandamano ya leo ya amani ni kuishinikiza serikali kuwajibika ukizingatia mauaji ya wanaharakati pamoja na ambao hawajulikani waliko. Kufikia sasa serikali imekiri kuwa idadi ya waandamanaji waliopoteza maisha yao ni 25 , ila takwimu za shirika la kitaifa la kutetea haki za binadamu KNCHR, inaelezea mauaji ya watu 41 na majeruhi 360.
Soma pia: Baadhi ya vijana hawajaridhishwa na Ruto kulivunja baraza la mawaziri
Kwa upande wake, kaimu inspekta mkuu wa polisi Douglas Kanja amewatahadharisha waandamanaji kuwa wakora wanapanga kuwavuruga. Kaimu Inspekta mkuu huyo wa polisi wa Kenya amewarai waandamanaji kudumisha utulivu na kushirikiana na maafisa wa usalama.
Saa chache zilizopita taarifa ya baraza la Makanisa limekashifu mauaji na kuelezea kuwa yanakiuka sheria. Askofu Antony Muheria ni wa kanisa la katoliki dayosisi ya Nyeri na anaamini ipo nafasi ya kufanya mabadiliko.
Haya yanajiri baada ya magunia ya maiti zisizopungua 8 kuopolewa timboni Kware mtaani Embakasi mwishoni mwa wiki iliyopita. Kwa sasa familia zimeombwa kujitokeza kutambua maiti hizo ambazo zinafanyiwa ukaguzi na upasuaji kwenye chumba cha hifadhi cha City. Mshukiwa mkuu amefikishwa mahakamani hii leo.
Huko Kisumu, waandamanaji wanasisitiza kuwa Lengo ni kuishinikiza serikali kuu kuwajibika na wala sio kuhangaisha uongozi wa serikali ya kaunti. Itakumbukwa kuwa baraza jipya la mawaziri Linasubiriwa na wito umetolewa kuwapa nafasi wataalam.
Yote hayo yakiendelea, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linaitolea wito shirika la fedha duniani, IMF, kufanya kazi kwa pamoja katika utekelezaji wa mpango wake wa kiuchumi na kutimiza haki za binadamu.
Soma pia: Kenya yashuka zaidi katika nchi zisizoweza kukopesheka
Ifahamike kuwa mswada wa fedha wa 2024 ukizingatia mpango huo wa IMF na Kenya, ulitarajia kukusanya dola bilioni 2.7 za Marekani za Pato la ziada katika mwaka mpya wa fedha ikiwa ni baadhi ya masharti ya IMF.