1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Mafuta na petroli zapanda bei kwa shilingi 20

15 Septemba 2022

Bei ya mafuta na petroli nchini Kenya imepanda kwa shilingi 20 zikiwa ni siku mbili tangu Rais William Ruto kutangaza kuwa ruzuku kwenye bidhaa za petroli itaondolewa.

Symbolbild Tankstelle
Picha: Vincent Mouchel/MAXPPP/dpa/picture alliance

Tangazo hilo linatimiza kigezo cha hazina ya fedha ya kimataifa, IMF,inayoishinikiza Kenya kusitisha mpango wa kutoa ruzuku kwa bidhaa za petroli ifikapo Oktoba mwaka huu.

Siku mbili baada ya rais William Ruto kutangaza kuwa bei ya mbolea itashushwa kwa nusu, bei ya mafuta na petroli imepanda kwa shilingi 20 hii leo.Haya yanajiri wakati ambapo Kenya inajitahidi kutimiza masharti ya Mfuko wa fedha ulimwenguni, IMF,ulioipa serikali mkopo katika utawala wa Uhuru Kenyatta.

Kwa sasa lita moja ya petroli itauzwa kwa shilingi 179 za Kenya kutokea 159 ambayo ni sawa na ongezeko la shilingi 20.Dizeli imepandishwa bei kwa shilingi 25 hadi 165 kwa jiji la Nairobi. Mafuta ya taa nayo yameongezwa bei kwa shilingi 20 na yatauzwa kwa shilingi 147.94 kwenye mji mkuu. Bei hizo zinajumulisha kodi ya ongezeko la thamani.

Bei hizo mpya zinaanza kutumika mara moja na zinaashiria kuwa ruzuku kwa bidhaa za petroli imefutiliwa mbali na kwa dizeli na mafuta ya taa imepunguzwa.

Kufikia sasa Kenya imeshatumia dola bilioni 1.2 ambayo ni sawa na 86% ya pato la utalii la mwaka huu, kugharamia ruzuku zinaeleza takwimu rasmi za serikali. Je wakenya wanasemaje kuhusu ongezeko la bei za mafuta?

Kupanda kwa bei ya mafuta Kenya

01:55

This browser does not support the video element.

Ongezeko hilo la bei ya mafuta huenda likaathiri shughuli za kilimo na kuongeza gharama zake ijapokuwa bei ya mbolea ilishushwa mwanzoni mwa wiki hii.Kuanzia wiki ijayo bei mpya ya mbolea inatarajiwa kuanza kufanya kazi.

Wakulima wa maeneo ya kaskazini mwa bonde la ufa wanaojikita kwenye kilimo cha mahindi wana mtazamo huu ukizingatia bei ya mbolea na pembejeo na hali halisi.

Kwa upande mwengine,bei ya umeme nayo pia imeongezeka kwa 15.7% na kubatilisha punguzo lililotangazwa mwanzoni mwa mwaka huu na rais aliyeondoka madarakani Uhuru Kenyatta.

Kwa mantiki hii,wateja wanaotumia zaidi ya vipimo 100 kwa mwezi vya umeme majumbani mwao watalipa zaidi. Viwanda na makampuni makubwa watakabiliana na bei kubwa zaidi za umeme kwani gharama za kusambaza huduma hizo zimeongezeka kwa zaidi ya thuluthi moja.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW