Kenya: Mahakama yasimamisha bomoabomoa Kariobangi
7 Mei 2020
Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja anaishinikiza serikali kutoa taarifa kamili ya kilichosababishwa ubomoaji kwenye mtaa wa Kariobangi wa Sewage. Kadhalika anashikilia kuwa haki za raia wasiokuwa na hatia sharti zitheshimiwe hata pale serikali inapoichukua ardhi yake.
Seneta Sakaja wa kaunti ya Nairobi kadhalika amesisitizia umuhimu wa kuipata ripoti kamili ya ardhi yote iliyotengewa ujenzi wa barabara na huduma za umma.
Haya yanajiri wakati ambapo wizara ya ardhi imefungua tena milango yake kuwahudumia wananchi baada ya chama cha mawakili nchini kupinga hatua hiyo. Afisi za wizara ya ardhi zilifungwa tangu mwishoni mwa mwezi wa Februari katika mazingira ya kutatanisha kabla ya kisa chochote cha COVID 19 kutangazwa.
Watu wapatao 5,000 wameathiriwa na zoezi hilo
Kwa upande wake, Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior anaitolea wito kamati ya muda inayoongozwa na Seneta Sakaja wa Nairobi kusaka mbinu za kuzisaidia zaidi ya familia alfu tano zilizoachwa bila makazi.
Yote hayo yakiendelea mahakama kuu imesitisha bomoa bomoa ya makazi ya mtaa huo wa Kariobangi hadi pale kesi iliyowasilishwa na kikundi cha Kariobangi Sewage Self Help Group itakapoamuliwa.
Wasisitiza ardhi hiyo ilipatikana kihalali
Wakaazi wa mtaa huo wa mabanda walio pia wanachama wa kikundi cha Sewage, wanashikilia kuwaserikali iliwapa ardhi hiyo.
Kauli za wakazi hao zinaungwa mkono na mwakilishi wa wadi ya Kariobangi Kaskazini, Julius Maina Njoka.
Mwakilishi huyo wa wadi alikamatwa na maafisa wa usalama alipopatikana kwenye eneo hilo akigawa chakula cha msaada. Wakazi wa mtaa wa mabanda wa sewage wanashikilia kuwa wameishi eneo hilo kwa miaka 12. Inasadikika kuwa ardhi hiyo imetengewa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha maji taka cha mtaa wa Dandora.
Thelma Mwadzaya, DW Nairobi.