1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Mchakato kumtafuta jaji mkuu mpya waanza Kenya

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Dw, Nairobi.12 Aprili 2021

Mchakato wa kumtafuta Jaji Mkuu Mpya nchini Kenya umeingia hatua mpya kwa kuwahoji wagombea wanaowania wadhifa huo kumrithi jaji mkuu aliyestaafu David Maraga.

Kenia Oberstes Gericht annuliert Wahlen
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. curtis

Jumla ya wagombea kumi, miongoni mwao majaji watano, mawakili na wabobezi wa sheria wanawania nafasi ya kumrithi Jaji David Maraga, aliestafu mwanzoni mwa mwaka huu.

Mchakato wa kujaza nafasi ya jaji mkuu wa 15 tangu taifa hilo kujipatia uhuru wake, umeanza kwa kumhoji Jaji Said Juma Chitembwe, ikiwa ni miaka miwili tu kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu.

Soma pia: Jaji mkuu wa Kenya ataka bunge livunjwe kwa kukosekana usawa wa kijinsia

Akijitetea mbele ya Tume hiyo Jaji Chitembwe amesema kuwa akipata nafasi hiyo atahakikisha kuwa kesi zinaamuliwa kwa kipindi cha mwaka mmoja, kinyume na ilivyo sasa, huku akiahidi kushirikiana na mihimili mingine ya uongozi kama Bunge na Rais.

Jaji wa zamani aliyestaafu Januari 2021 David Maraga.Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Jaji mstaafu David Maraga aliyeonekana kukwaruzana na Rais kuhusu masuala ya maamuzi na kuzingatia katiba, kila mara alinukuliwa akisema kuwa kesi zilikuwa zinarundikana mahakamani, kwa sababu ya raslimali chache ambazo serikali kuu iliitengea Idara ya Mahakama.

Je, Tume inayooendesha mahojiano haya iko huru kiasi gani?

Ukilinganisha taifa la Kenya na mataifa mengine ya kanda hii kuhusu mchakato wa kumchagua Jaji Mkuu, Musa anasema kuwa Kenya inaongoza, licha ya kuwa na changamoto za hapa na pale. Rais ndiye mwenye mamlaka ya kumchagua Jaji Mkuu katika Mataifa ya Afrika Mashariki kinyume na Kenya. Baadhi ya wachambuzi wamehoji kwamba mahakama pamoja na tume ya mahakama imekuwa huru nchini Kenya, na ndiyo sababu mahakama ya juu iliweza kufanya uamuzi w akubatilisha ushindi wa rais Uhuru Kenyatta mwaka 2017. 

jumla ya watu kumi wameorodheshwa kuhojiwa kuwania nafasi ya jaji mkuu wa Kenya.Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Jaji Mkuu huteuliwa na Rais, kutoka miongoni mwa majina matatu yanayopendekezwa kwake na Idara ya mahakama, baada ya kuhojiwa na makamishna wa Tume ya Idara ya Mahakama. Hata hivyo mchambuzi Martin Andati anatofautiana na mwenzake Musa kuhusu uhuru wa Tume ya Idara ya Mahakama, akihoji uhuru huo haujatimia itakikanavyo na kwamba kuna mgongano wa kimaslahi.  

Jaji anayetafutwa lazima awe amehitimu shahada ya sheria kwenye chuo kikuu, anatimiza vigezo vilivyoainishwa katika ibara sita ya katiba kuhusu uadilifu na amehudumu kwenye Nyanja ya sheria kwa kwa kipindi cha miaka 15. Mchakato huu utakamilika baada ya majuma mawili.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW