Kenya miongoni mwa nchi zinazoboresha magereza
8 Juni 2022Hatua muhimu katika kuyafanya magereza kuwa vituo vya kurekebisha tabia ni kuhakikisha kwamba miundo mbinu imeboreshwa. Akizungumzia mageuzi kwenye idara ya magereza, Waziri wa teknolojia na mawasiliano, Joe Mucheru amesema mataifa mengi yanashuhudia vitisho kutoka kwa makundi yenye itikadi kali na nimuhimu kuzingatia hili katika kuyafanya magereza salama.
"Ni muhimu kwetu kama serikali, kubadili namna mifumo yetu ya magereza inavyofanya kazi, na kuvifanya vituo vya urekebishaji tabia, kuhimiza utangamano wa kijamii na kuyajenga upya maisha. Uboreshaji wa gereza la Shimo la Tewa, umeinua hali ya maisha ya washukiwa wa uharamia, waliokuwa wanasubiri kufunguliwa mashtaka, kulingana na viwango vya kimataifa.”
Usimamizi wa magereza unaonesha kuwa asilimia 80 ya wafungwa ni watu wenye tija, wakiwa vijana na watu wa umri wa wastan. Serikali inabuni mbinu za kuhakikisha kwamba wanahusika katika kuchangia uchumi wa taifa la Kenya. Msimamizi wa ujumbe wa kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu, Daniel Gerald ameelezea kujitolea kwao katika kuboresha magereza ya mataifa wanachama barani Afrika. "Kwa upande wa usaidizi kwenye kanda hii tuna mipango ya kuujumuisha Umoja wa Afrika, AU, tunawapa mapendekezo yetu kuhusu matatizo ya ufadhili na uungwaji mkono wa kisiasa ambao huduma za magereza zinahitaji.”
Serikali imeahidi kufanya kazi na wadau wengine kwenye idara ya magereza kuona kwamba kupitia mfumo wa kutumia njia m'badala ya kutatua mizozo idadi ya wafungwa wanaohukumiwa kutumikia kifungo jela, imepungua. Akizungumza na idhaa hii Hakimu Joel Ngugi wa mahakama kuu jijini Nakuru ameeleza kwamba:
"Mfumo huu unawapa wahusika wote fursa ya kuangalia malalamiko yao kwa kina, kuzungumza, na vile vile wapatanishi wanapata kubuni mbinu mbalimbali za kurejesha mahusiano yaliyokuwa yamepotea. Hili ni jambo ambalo mahakama haiwezi kufanya.”
Wiki iliyopita Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliwaachia huru wafungwa 3,908, kufuatia pendekezo la kamati ya mahakama inayoshauri kuhusu msamaha wa Rais kwa wafungwa. Rais aliitaja hii kama fursa yingine ya kuyaimarisha Maisha yao na akawataka kukumbatia na kuhimiza mabadiliko kwenye jamii.
Wakio Mbogho, DW, Nakuru.