Kenya: Muungano wa upinzani, NASA wasambaratika
30 Julai 2021Siasa za nchini Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 zinazidi kushika kasi. Muungano wa NASA unasambaratika, huku muungano mpya wa Okoa Kenya Alliance ukikabiliwa na misukosuko kwa kuwa wadau watarajiwa bado hawajafikiana kuhusu mustakabali wao. Chama tawala cha Jubilee nacho kiko kwenye harakati za kumnadi kiongozi wa ODM Raila Odinga katika eneo la Mlima Kenya.
Muda mfupi uliopita chama cha Orange Democratic Movement, ODM kilitangaza kujiondoa rasmi kwenye muungano wa upinzani wa NASA ambao umekuwa ukiregarega. Tofauti zilijiri baada ya mzozo wa kugawa ruzuku ya vyama vya kisiasa kuzuka. Kwa sasa ODM inatishia kutowagawia wadau wa NASA ruzuku hiyo ya jumla ya shilingi milioni 153. Kwenye kikao cha baraza kuu la ODM, wanachama wanawarai wadau kubadili mitazamo yao.
Edwin Sifuna ni katibu mkuu wa chama cha Orange Democratic Movement ODM anasisitiza kwamba "Ishu ya pesa ndani ya NASA tumeshaimaliza, lakini wenzetu wameondoka ndani ya chama muungano wa NASA. NASA haiko tena, na kuna uwezekano kama vile ilivyofanyika 2002, kuwe na miungano ya miungano."
Ifahamike kuwa ili muungano huo wa NASA ulioundwa 2017 usambaratike kisheria, sharti vyama vitatu vijondoe rasmi kwa kumtaarifu msajili wa vyama. Duru zinaeleza kuwa kiongozi wa Wiper iliyomeguka mapema wiki hii, Kalonzo Musyoka yuko kwenye harakati za kufanya mazungumzo ya kina yatakayoamua hatima yao kisiasa.Kimsingi kiongozi wa ODM Raila Odinga sasa yuko kwenye jukwaa moja na mwenzake wa KANU Gideon Moi. Chama cha KANU kinaegemea upande wa chama tawala cha Jubilee. Hata hivyo viongozi wake wanashikilia kuwa hawajafikia mwafaka na yeyote kisiasa.Nick Salat ni Katibu Mkuu wa KANU na analisisitizia hilo.
"Kina Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka waheshimu huu mkataba tulionayo na nini, na Jubilee, si ndio!.... na hatukatai kuungana na hawa."
Muungano mpya wa Okoa Kenya, OKA, ambao haujarasimishwa unawaleta pamoja viongozi wa KANU, Gideon Moi, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Moses Wetangula wa Ford -Kenya na Musalia Mudavadi wa ANC.Duru zinaashiria kuwa kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi anang'ang'ania kuwa mpeperusha bendera ya muungano wa Okoa Kenya jambo ambalo linazua mitazamo tofauti.
Yote hayo yakiendelea washirika wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta wanaotokea eneo la Mlima Kenya wanafanya kikao hii leo kuandaa mikakati ya kumnadi kiongozi wa Orange Democratic Movement,ODM Raila Odinga kwa wakaazi wa eneo la kati.Hii ni mara ya kwanza kwa wanasiasa wa eneo hilo kuja pamoja kumpa ridhaa Raila Odinga kuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta.Mpango huo una azma ya kukabiliana na naibu wa Rais William Ruto anayeendelea kunadi sera zake kwenye eneo hilo la Mlima Kenya anakotokea Rais Uhuru Kenyatta.