1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya na Tanzania zatia mikataba ya kibiashara na uwekezaji

Shisia Wasilwa, DW, Nairobi 4 Mei 2021

Kenya na Tanzania zimetia sahihi mikataba kadhaa ikiwemo ya kibiashara, uwekezaji na mahusiano kwa lengo la kuboresha ushirikiano na urafiki kati ya mataifa hayo ya Afrika Mashariki.

Kenia Nairobi | Besuch Samia Suluhu Hassan, Präsidentin Tansania | mit Uhuru Kenyatta
Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Akizungumza baada ya mazungumzo kati yake na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, Rais Samia Suluhu amesema kuwa atafanya juhudi kuona kuwa Watanzania wanajitahidi kujaza pengo la kibiashara kati ya mataifa hayo.

Rais Samia Suluhu Hassan anazuru Kenya takribani mwezi mmoja na nusu baada ya kuchukua hatamu za uongozi nchini Tanzania. Ziara yake ya pili nje ya Tanzania baada ya kuzuru Uganda majuma matatu yaliyopita, inaonekana kuwa mwamko mpya wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo jirani ya Afrika Mashariki ambayo hayajakuwa na mahusiano mema, chini ya rais John Pombe Magufuli aliyeaga dunia.

Alipowasili mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta alimkaribisha katika Ikulu ya Nairobi alikagua gwaride la heshima na kupigiwa mizinga 21 kabla ya kufanya mazungumzo. Kenya ni mwekezaji mkuu wa tano nchini Tanzania, ikiwa ya kwanza katika jumuiya ya Afrika Mashariki.

Rais Samia Suluhu Hassan awasili Kenya

This browser does not support the audio element.

"Tanzania tutakuja kwa nguvu zote Kenya ili kuwekeza na ili kukuza ujazo wa biashara,” amesema Rais Samia.

Kenyatta na Samia wakubaliana kuondoa vikwazo vya kibiashara mipakani

Bishara na uwekezaji kati ya Kenya na Tanzania ni wastan wa dola milioni 450 za Marekani, huku Kenya ikiuza bidhaa nyingi zaidi ya Tanzania. Hata hivyo marais hao wamekubaliana kuondoa vikwazo kwenye mipaka ili kurahisisha biashara kati yazo. Aidha wamewataka matabibu kwenye mipaka kurahisishia wafanyibiashara kuingia na kutoka kwenye mataifa hayo wanapowapima watu ugonjwa wa covid-19.

Mahusiano ya m kwaruzano kati ya Kenya na Tanzania

Kenya na Tanzania zimekuwa na mahusiano yenye mikwaruzano ya mara kwa mara, huku kila taifa likituhumu mwenzake kwa mbinu chafu za kibiashara. Hata hivyo ujio wa Rais Samia Suluhu Hassan unaashiria mabadiliko ya sera za mtangulizi wake Hayati Rais John Pombe Magufuli. Ziara yake Suluhu inajiri wakati taifa hilo likitia sahihi mkataba na Uganda wa dola bilioni 3.5 ya bomba la mafuta.

"Tumekubaliana kwamba na tumeweka mkataba, wa kujenga bomba la gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa, hiyo itarahisisha bei ya stima na kusaidia, viwanda vyetu kupata nishati safi,” amesema Rais Kenyatta.

Gwaride la heshima lililoandaliwa na wanajeshi wa Kenya katika ikulu ya rais jijini Nairobi kwa heshima ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania 04.05.2021.Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Baadhi ya masuala yenye utata ambayo yamevuruga mahusiano kati ya Kenya na Tanzania ni udhibiti wa bidhaa za kilimo. Hivi majuzi Kenya ilipiga marufuku ununuzi wa mahindi kutoka Tanzania na Uganda kwa kile ilichosema ni viwango vya juu vya kuvu.

Mwaka 2017, Tanzania ilipiga marufuku ununuzi wa vifaranga 6,000 kutoka Kenya kwa sababu ya wasiwasi wa kusambaa kwa homa ya ndege. Wachambuzi wa masuala ya kidiplomasia wanasema kuwa heshima na taadhima kwa Rais Samia, ni dhihirisho la mwelekeo mpya wa kufanya biashara na ushirikiano kati ya mataifa hayo.