1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya na Uganda kujenga njia ya reli

Kabogo Grace Patricia7 Januari 2009

Kenya na Uganda zina mpango wa kujenga njia mpya ya reli kutoka katika bandari ya Mombasa kwa lengo la kukabiliana na ongezeko la biashara baina ya nchi za Afrika Mashariki na nchi jirani zisizo na bandari.

Rais wa Kenya Mwai Kibaki, (katikati), akiwa na Waziri Mkuu, Raila Odinga, (kulia) wakati wa upatanishi uliofanywa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, (shoto), kutokana na machafuko baada ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo, wakiahidi kufanya kazi kwa pamoja kuijenga Kenya.Picha: AP


Nchi hizo mbili kwa sasa zinaunganishwa na reli iliyojengwa mwanzoni mwa karne ya 20 na maafisa wanasema njia hiyo inasafirisha chini ya asilimi 6 ya bidhaa zinazokwenda ndani ya Kenya na nchi nyingine za eneo la Afrika Mashariki.


Waziri wa usafiri wa Kenya, Chirau Ali Mwakwere, amesema ubora wa reli hiyo mpya ina umuhimu sio tu kwa uchumi wa nchi hizo mbili, bali pia kwa uchumi wa nchi zisizo na bandari katika eneo hilo.


Akizungumza wakati wa mkutano wa maafisa wa serikali za Uganda na Kenya, Mwakwere amesema kuwa bandari ya Mombasa hupokea tani milioni 16 za mizigo kwa mwaka na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia tani milioni 30 kwa mwaka ifikapo mwaka 2030.


Kwa mujibu wa Mwakwere, Kenya na Uganda zitafanya upembuzi yakinifu wa dola milioni 10, ambapo Kenya itatoa kiasi cha dola milioni 8 na Uganda itatoa kiasi kilichobakia. Fedha hizo zinatarajiwa kutoka katika bajeti za mwaka wa fedha 2009/2010 za nchi hizo mbili.


Aidha, Waziri wa Kazi na Usafiri wa Uganda, John Nasasira amesema njia ya reli inayotumika kwa sasa imepitwa na wakati, ingawa wanaamini kuwa ujenzi wa njia mpya utawezekana. Amesema njia hiyo ya reli itakayokamilika mwaka 2017, itakwenda hadi Rwanda, Ethiopia, Sudan ya Kusini na Burundi.


Mwishoni mwa mwaka 2007 njia hiyo ya reli inayoishia kwenye mji mkuu wa Uganda, Kampala ilikuwa ikisafirisha chini ya asilimia 6 ya mizigo iliyosafirishwa katika barabara ya kaskazini inayounganisha Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, baadhi ya sehemu za Tanzania, Sudan ya Kusini na Ethiopia. Barabara kuu kutoka Mombasa hadi kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi ambayo inaelekea mpaka Kampala, inatumiwa kwa wingi na malori makubwa ya mizigo.


Kwa miaka kadhaa utendaji mbovu nchini Kenya na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Uganda, yalisababisha serikali hizo mbili kukumbwa na matatizo ya ununuzi wa vipuri na kuikarabati njia ya reli ya sasa pamoja na treni.


Shirika la reli la Rift Valley, linaloongozwa na kampuni ya Afrika Kusini ya Sheltam, lilishinda zabuni ya kuendesha shirika la reli la Kenya na Uganda kwa pamoja kwa muda wa miaka 25 kuanzia Novemba, mwaka 2006. Kampuni hiyo iliahidi kuongeza usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli kutoka asilimia 20 ya mizigo iliyokuwa ikihifadhiwa katika bandari, lakini uwezo wake umekuwa ukishuka tangu wakati huo.


Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga akizungumza kwenye mkutano huo, alisema njia za reli zinazounganisha nchi hizo kwa sasa zimepitwa na wakati kwa kuwa zilijengwa zamani na kwamba ni kikwazo kikubwa kwa biashara.




Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW