KENYA NA WANARIADHA WAKE WANAO BADILI URAIA:BUNDESLIGA NA CHAMPIONS LEAGUE:
14 Aprili 2005-BUNDESLIGA:
Kufuatia changamoto za mwishoni mwa wiki iliopita,Bayern Munich iliopigwa kumbo nje ya champions League kati ya wiki hii na Chelsea ya Uingereza, ilifungua mwanya wa pointi 3 kati yake na Schalke 04.Timu hizi mbili kitambo zilikuwa sawa kwa pointi kileleni,lakini Schalke iliteleza jumamosi iliopita ilipozabwa mabao 4:0 na Stuttgart.Kwa msaada huo kutoka Stuttgart na ushindi wake wa mabao 2:1 dhidi ya Borussia Mönchengladbach,B.Munich ilifungua mwanya wa pointi 3.Mabingwa Bremen wananyatia bao nafasi ya 4.Munich lakini,ilijitapa kwamba ingechukua vikombe vyote 3 msimu huu-viwili nyumbani na kimoja cha Ulaya.Lakini ndoto hiyo sasa imetoweka.Klabu zote 3 za Ujerumani zilizokua zikiania Kombe hili msimu huu zimepigwa kumbo.
CHAMPIONS LEAGUE:
Katika duru ya pili ya robo-finali ya Champions League-Kombe la klabu bingwa barani Ulaya kati ya wiki hii,Liverpool ya Uingereza iliitoa Juventus ya Itali na kuweka miadi na Chelsea katika nusu-finali ya Kombe hilo.
Liverpool ya Uingereza ilizima vishindo vya Juventus mjini Turin na mwishoe ikaitoa kwa mabao 2:1 iliotia duru ya kwanza.Sasa Liverpool ina miadi na Chelsea ilioipiga kumbo Bayern Munich ya Ujerumani.
Kikundi cha mashabiki 50 wa Juventus kilipambana na polisi ya Itali nje ya uwanja wa Delle Alpi Stadium mjini Turin muda mfupi kabla ya dimba kuanza. Mashabiki hao walikua sehemu ya kundi kubwa la kiasi ya mashabiki 150 waliojiwinda kupambana na Polisi na kuwarushia makombora.Mashabiki wa Juventus wakihofiwa kutaka kulipiza kisasi kwa msiba wa 1985 uliotokea katika Uwanja wa Heysel Stadium,mjini Brussels pale timu hizi 2 zilipokutana.Mashabiki 39 wengi wao wa Juventus walifariki baada ya ukuta kuanguka kwa vurumai iliosababishwa na mashabiki wa Liverpool.
PSV Eindhoven ya uholanzi, mabingwa wa Ulaya 1988,wameipiga kumbo Olympic Lyon ya Ufaransa kwa mabao 4:2 kufuatia changamoto za mikwaju ya penalty baada ya mchezo kurefushwa.
Eindhoven na Olympique Lyon zilitoka suluhu bao 1:1 kabla mikwaju ya adhabu ya penalty kuamua hatima ya mpambano huu.
KOCHA WA UJERUMANI :
Kocha wa Timu ya taifa ya ujerumani-Jürgen Klinsmann alisema wiki hii kwamba hana hamu ya kuzungumzia kurefushwa kwa mkataba wake kwani hataki kushughulishwa na jambo jengine ikiwa aiongoze Ujerumani kutwaa Kombe la dunia 2006.
Klinsmann ana mkataba hadi kumalizika Kombe la dunia 2006 lakini Shirikisho la dimba la Ujerumani (DFB) linaripotiwa lina hamu kuzungumza nae juu ya kurefusha mkataba huo.
Klinsmann alishika wadhifa huu kutoka kwa Rudi Völler baada ya Ujerumani kuaibishwa katika Kombe la Ulaya la mataifa mwaka jana huko Ureno.Turufu yake kubwa tangu kuwa kocha wa ujerumani ni kuwapa nafasi chipukizi kama vile mlinzi wa Chelsea,Robert Huth na Thomas Hitzlsberger wa Aston villa pamoja na Lukas Podolski wa timu ya daraja ya pili ya FC Cologne.
Klinsmann alieibuka bingwa wa dunia na Ujerumani 1990,chini ya kocha Franz Beckenbauer,mwenyekiti wa sasa wa Kamati ya maandalio ya Kombe lijalo la dunia, anataka kuiona Ujerumani inalitwaa tena kwa mara ya 4 Kombe hilo la dunia baada ya 1954 mjini Berne, uswisi;1974 nyumbani Ujerumani na 1990 m jini Roma,Itali.
Kombe lijalo la dunia litaanza Juni 9 na kumalizika Julai 9.
RIADHA:Wakuu wa chama cha riadha cha Kenya wameuhoji mpango uliotangazwa kati ya wiki wa kutaka kuwaondosha nchini Kenya wanariadha wa asili ya nchi hiyo waliobadili uraia ili kukimbia chini ya bendera ya mataifa mengine.
Maafisa wa chama hicho cha riadha wameripotiwa kusema amri ya waziri wa michezo wa Kenya Ochilo Ayacko kuwatimua nchini wanariadha kama hao endapo wakikutikana wanafanya mazowezi nchini, yamkinika isiweze kutekelezwa kisheria na waweza pia kuzusha athari za kibalozi.Afisa mmoja wa hadhi ya juu wa chama cha riadha cha Kenya, amenukuliwa kusema kuwa, kuna wanariadha wengi wanaokwenda Kenya kwa mazowezi kila mwaka.
Mkuu huyo alisema kuwa wingi mkubwa wa halmashauri ya wajumbe 12 ya chama cha riadha cha Kenya wanaungamkono maoni yake na wanataka kukutana haraka na waziri Ayako kuzungumzia swali hilo.
Waziri wa michezo aliamrisha jumaane iliopita kukabidhiwa hadi wiki hii ijayo orodha ya majina ya wanariadha wa Kenya waliochukua uraia wa mataifa mengine ili awachukulie hatua watakapojaribu kufanya mazowezi yao nchini Kenya.
Waziri Ayacko ambae amekuwa akijaribu kuzima wimbi la wanariadha wa Kenya wanaogeukia kukimbia kwa niaba ya nchi nyengine ,aliwahi kutoa taarifa kama hizo hapo kabla na hata desemba mwaka jana ,lakini hakuna kitendo kilichochukuliwa.
Ahadi yake ya hivi sasa kuchukua hatua aliitoa katika mkesha wa tangazo la jumatano la stadi wa Kenya wa mita 1500,Bernard Lagat kuwa amechukua uraia wa Marekani.
Bernard Lagat ni bingwa wa olimpik wa medali ya shaba huko Sydney, 2000 katika masafa ya mita 1500.Lagat aliipatia pia Kenya medali ya fedha katika michezo iliopita ya olimpik mjini Athesn, Ugiriki.Lagat katika washington University.Lagat alisema kutoka nyumbani kwake huko Tucson,Arizona,kwamba hakupitisha uamuzi huo kwa urahisi hatahivyo anakusudia kuseleleza mafungamano makubwa na Kenya.
Bernard lagat ni mmoja tu kati ya jumla ya wanariadha kiasi cha 12 wa Kenya waliobadili uraia kukimbia chini ya bendera za kigeni.Wengi wao wamekwenda nchi nono za mafuta za ghuba kwa sababu za kiuchumi.
Wa kwanza alikua Sammy Kipketer, alieipatia Danmark medali ya dhahabu katika mashindano ya ubingwa wa riadha wa dunia.
Mwengine ni Stephen Cherono, ambae kwa jina la Saif Shaheen ambae aliipatia Qatar medali ya dhahabu 2003 katika ubingwa wa riadha duniani.
Hatua hizi za wanariadha hao wa Kenya zimezusha mjadala motomoto nyumbani Kenya,hasa kwavile wengi wao hurejea nyumbani Kenya,nchi ya asili kwa mazowezi kwa mashindano makuu ya kimataifa.
Kenya ambayo inadai medali ya dhahabu ya mita 3000 kuruka viunzi ni mali yake hasa katika olimpik, ilimzima Saif Saeed Shaeen,kushiriki katika michezo iliopita ya Olimpik huko Athens,kwa kuhofia ule wembe uliowanyoa katika ubingwa wa dunia usiwanyoe tena katika Olimpik.
Lakini je, ni haki kuwazuwia wanariadha wasipiganie tumbo lao badala ya bnendera yao ?Wanariadha wengi wa Kenya miaka ya 1970ini walitikisa dunia kutokana na kujifunza Marekani na kutumia zana za michezo katika vyuo vikuu vya Marekani-Miongoni mwao ni Dr.Mike Boit,aliejifunzia huko Durham, North Carolina.
Tukiacha ubishi huu unaendelea, bingwa wa rekodi ya dunia kutoka Kenya-Paul Tergat,ataingia barabarani kesho jumapili kukimbia katika London marathon,kwa niaba yake na Kenya.Tergat alieweka rekodi ya dunia mwaka juzi mjini Berlin,ameahidi kuivunja rekodi yake hiyo ya masaa 2,dakika 4 na sek.55.
Bingwa huyu mara 5 wa dunia wa mbio za nyika anaetazamiwa kushinda mbio za jumapili zikiwa za 25 za London marathon. Katika shabaha yake ya kuvunja rekodi yake, alisema kuna mambo mengi kuzingatia: Kuna hali ya hewa itakavyokua na jinsi gani waliowanaotangulia kumtilia kasi watakavyomudu kupambana na hali hiyo.
Inatabiriwa kuwa hali ya hewa jumapili mjini London itakua bila ya rasha-rasha za kawaida.Mkenya mwengine katika mbio hizo atakuwa
Silas Kirui ambae ndie atakaemtilia Tergat kasi.Hasimu mkubwa wa Paul Tergat atakuwa mtaliana Stefano Baldini, kijana kwa miaka 2 kuliko Tergat.
Mshindi wa mwaka jana wa London marathon ni Evans Rutto ambae alikosa kushiriki katika mbio za olimpik za Athens na amewasili London kutetea taji lake.Ruto amekuwa akifanya mazowezi huko Colorado,Marekani kwa azma ya kushindajumapili.Anatumai tu kuwa hali ya hewa itakua bora zaidi kesho kuliko ilivyokua mwaka jana.