1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Ni haramu kutumia magenge ya uhalifu kisiasa

16 Februari 2026

Waziri wa Usalama Kenya, Kipchumba Murkomen ametoa onyo kuhusu kurejea kwa magenge ya uhalifu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027 , akiwashutumu baadhi ya wanasiasa kwa kufadhili makundi hayo.

Kenia | Ein kenianisches Gangmitglied hält eine Machete fest
Waziri wa usalama Kenya Kipchumba Murkomen amesema baadhi ya wanasiasa wanafadhili makundi ya uhalifu ili kuvuruga mikutano ya kisiasa ya wapinzani wao.Picha: DW

Waziri Kipchumba Murkomen ameibua wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa vijana katika mitandao ya uhalifu, hasa katika maeneo ya mijini na makazi yenye msongamano mkubwa wa watu. Ametaja hasa kuibuka kwa kundi linalojulikana kama "Team Mbogi”, lililoanza kujitokeza mwaka 2025 na ambalo limekuwa likifanya shughuli zake katika baadhi ya maeneo ya Nairobi, Kenya. Watu waliokamatwa kuhusiana na genge hilo walikuwa na umri wa kati ya miaka 13 na 22, hali ambayo Waziri aliieleza kuwa ni ishara ya kutisha ya kuongezeka kwa ushiriki wa watoto na vijana katika uhalifu uliopangwa.

Akizungumza bungeni alipofika kujibu maswali kuhusu hali ya usalama nchini, Murkomen alisema magenge ya uhalifu yamechochewa na mambo kama ukosefu wa ajira, utoro shuleni, matumizi ya dawa za kulevya na vurugu za kisiasa—kauli inayozua mjadala kuhusu uhusiano kati ya siasa na uhalifu:

"Wamiliki wa magenge wako ndani ya bunge hili; wengine wako Seneti na wengine katika ofisi za juu za vyama vya siasa. Hali hii haitakoma. Baadhi ya magenge ni yenu, mengine yameandikishwa na wapinzani wenu wa kisiasa. Ni muhimu sote tushughulikie tatizo hili la kimfumo la magenge kwa sababu linabadilika kila mara. Huanzia kama walinzi wa kisiasa, kisha wahuni wa kampeni, na hatimaye hugeuka magenge ya uhalifu.”

Waziri wa usalama Kenya, amezungumza bungeni akisema magenge ya uhalifu yamechochewa na mambo kama ukosefu wa ajira, utoro shuleni na matumizi ya dawa za kulevya mingoni mwa mambo menginePicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Katika Kaunti ya Baringo, zoezi la kuwanyang'anya raia silaha haramu linaendelea huku wakazi wakilalamikia mashambulizi ya mara kwa mara. Kaunti za Kilifi, Siaya na maeneo ya Magharibi mwa Kenya pia zimeripoti visa vya mashambulizi vinavyohusishwa na magenge.

Polisi yaongoza operesheni ya kuwasaka wahalifu 

Katika kaunti ya Mombasa, mashambulizi ya mapanga yamewaacha wakazi wakiishi kwa hofu. Mapema mwezi huu, Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) pamoja na viongozi wa usalama wa kikanda waliongoza operesheni dhidi ya makundi hayo yanayojulikana kama "panga boys.” Kamanda wa Polisi eneo la Pwani, Ali Nuno, alitoa agizo linalowaruhusu maafisa kutumia silaha dhidi ya washukiwa wenye silaha wakati wa operesheni za usalama:

"Wakati unachukua panga yako na unataka kumshambulia mwananchi, nimetoa amri ya kutosha maafisa watumie silaha zao, na hao vijana wanaofanya uhalifu waangushwe mmoja baada ya mwingine mradi tu sheria inaturuhusu.”

Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) pamoja na viongozi wa usalama wa kikanda wanaongoza operesheni dhidi ya makundi ya wahalifu yanayojulikana kama "panga boys.” Picha: Luis Tato/AFP/Getty Images

Maseneta pia waliibua hoja hizi bungeni. Waliunga mkono kauli ya Waziri wakisema wana ushahidi kuwa baadhi ya wanasiasa wanafadhili makundi hayo. Wamemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi kueleza hatua zinazochukuliwa kukomesha hali hiyo. Seneta wa Nandi, Samson Cherargei, alisema:

"Msichana aitwaye Sheryi alipigwa risasi juzi Makadara, Nairobi. Nilishangaa kuona kwenye video watu wenye mapanga wakivamia duka Mombasa. Hata Haiti mambo kama hayo hayaonekani. Lazima kuwe na mkakati wa kupambana na magenge ya uhalifu. Tuliuliza Inspekta Jenerali alipofika mbele ya Kamati ya Seneti ya uhasibu wa Umma, kwa nini mnaruhusu magavana kuunda timu za maafisa wa utekelezaji wa sheria za kaunti wanaogeuzwa kuwa kama wanamgambo wadogo kwa maslahi yao ya kisiasa?”

Waziri Murkomen anadai kuwa kuingiliwa kwa siasa kumedhoofisha juhudi za polisi, akisema baadhi ya viongozi huwatisha maafisa au kudai wahamishwe wanapowakamata wahalifu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW