1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya, Tanzania kutatua mvutano sekta ya usafiri wa anga

16 Januari 2024

Kenya na Tanzania zimesema zinafanya juhudi kuutatua mvutano uliozuka baina ya nchi hizo mbili baada ya Tanzania kutangaza kufuta kibali cha safari za ndege za shirika la Kenya Airways kati ya Nairobi na Dar es Salaam.

 Ndege za Shirika la Kenya Airways| Uwanja wa Jomo Kenyatta, Nairobi
Shirika la Ndege la Kenya Airways ni miongoni mwa yale makubwa kabisa barani Afrika. Picha: Billy Mutai/AA/picture alliance

Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Tanzania, TCAA,  ilitangaza mnamo Jumatatu jioni kufuta kibali hicho kwa ndege za shirika hilo la Kenya kujibu msimamo wa serikali mjini Nairobi wa kukataa kutoa kibali cha kuingia Kenya kwa ndege za mizigo za kampuni ya ndege ya Tanzania.

Tangazo la TCAA lilisema ndege zote za Kenya Airways kutokea Nairobi hazitaruhusiwa kutua mjini Dar es Salaam kuanzia Januari 22.

Hata hivyo Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa nchi hizo mbili, wamesema wamefanya mawasiliano kwa njia ya simu na kukubaliana kuutafutia ufumbuzi mvutano uliojitokeza katika kipindi cha siku tatu zinazokuja.

Mawaziri hao January Makamba wa Tanzania na mwenzake wa Kenya, Musalia Mudavadi, wamethibitisha taarifa hizo kupitia ujumbe katika kurasa zao za mtandao wa kijamii wa X zamani ukijulikana kama Twitter.

Makamba amesema wamekubaliana na Mudavadi kwamba "vizuizi vya usafiri wa anga kati ya nchi zetu" na kutoka miongoni mwa nchi hizo kwenda nchi nyingine haupaswi kuwepo.

Ujumbe wa January Makamba

Ujumbe sawa na huo umetolewa na pia na Mudavadi akisema "hakuna sababu ya kuwepo wasiwasi" kwa sababu tayari wamekubaliana na Makamba kuwa mamlaka za usafiri wa anga za pande zote zitafanya kazi kutatua mvutano uliojitokeza.

TCAA yasema uamuzi wake dhidi ya Kenya Airways ulikuwa ni wa ´kujibu mapigo´

Shirika la Ndege la Kenya Airways hufanya safari za kila siku kati ya Nairobi na Dar es Salaam, Tanzania.Picha: picture-alliance/dpa

Katika taarifa ya awali ya TCAA, mamlaka hiyo ilisema uamuzi wa kuzuia ndege za Kenya Airways ulikuwa ni ´kujibu mapigo´ kwa msimamo wa Kenya kuzuia ndege za mizigo za Air Tanzania.

TCAA imesema Kenya iliinyima Air Tanzania kibali kwa ndege zake za mizigo kufanya safari baina ya nchi hizo mbili na kutoka Kenya kwenda nchi nyingine.

Kulingana na mamlaka hiyo, msimamo huo wa Kenya ni kinyume na makubaliano kati ya nchi hizo mbili kuhusu sekta ya usafiri wa anga yaliyotiwa saini mwaka 2016.

Baadaye kampuni ya ndege ya Kenya Airways ilitoa tamko ikisema inafahamu juu ya uamuzi uliochukuliwa na TCAA lakini ilikuwa inafanya mashaurino na mamlaka za nchi zote mbili "kutafuta suluhu na kuhakikisha hakuna mparaganyiko wa ratiba utakaotokea kwa safari za ndege kati ya Nairobi na Dar es Salaam."

Mvutano Kenya na Tanzania waongeza joto la misuguano Jumuiya ya Afrika Mashariki

Katika miaka ya karibuni, Tanzania imewekeza sana kulifufua shirika lake la ndege , Air Tanzania. Rais Samia Suluhu Hassan wa nchi hiyo, hutumia ndege za Air Tanzania kwa safari za ndani na kimataifa.Picha: Shisia Wasilwa/DW

Kenya Airways ni moja kati ya mashirika makubwa ya ndege barani Afrika. Tanzania, iliyo na vivutio vingine vya kitalii ikiwemo mbuga za wanyamapori, fukwe na milima, ni moja kati ya masoko makubwa ya kampuni hiyo ya Kenya.

Katika miaka ya karibuni Tanzania imekuwa ikijaribu kutanua usafiri wake wa anga kupitia kampuni ya taifa ya Air Tanzania ikianzisha safari za kikanda ikitumia ndege mpya zilizonunuliwa na serikali. Hivi karibuni pia ilipokea ndege mpya ya mizigo ikiwa ni juhudi za kuwania mapato ya sekta ya usafirishaji kwa njia ya anga barani Afrika.

Mvutano uliojitokeza jana ni wa hivi karibuni kabisa miongoni mwa mataifa wanachama 8 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hapo kabla Kenya ilitangaza kuzuia ungizaji maziwa kutoka Uganda na mazao ya kilimo kutoka Tanzania.

Tanzania nayo ilizuia kuingizwa vitunguu kutoka Kenya uamuzi uliosababisha kupanda kwa bei ya zao hilo muhimu.

Kwenye mzozo mwingine, hivi karibuni Uganda iliishtaki Kenya kwenye Mahakama ya Afrika Mashariki kwa kuinyima kibali kampuni ya mafuta ya Uganda cha kusimamia usafirishaji mafuta kutoka bandari ya Kenya ya Mombasa kwenye Kampala.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi