1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiAfrika

Kenya, Uganda na Tanzania zawasilisha bajeti zake

Lubega Emmanuel | Deo Kaji Makomba
15 Juni 2023

Baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Uganda, Kenya na Tanzania, zimewasilisha bajeti zake kwa mwaka mpya wa kifedha, katika wakati ambao gharama za bidhaa zimepanda maradufu.

Kenia Haushalt 2023 | Finanzminister Njuguna Ndung'u
Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Tanzania kutumia Trilioni 44 mwaka ujao

Tukianzia huko Tanzania serikali imewasilisha bajeti yake na imesema kuwa inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 44 nukta 39 katika bajeti yake kuu kwa mwaka wa fedha wa 2023/ 2024.

Kauli hiyo ya serikali ya Tanzania kukusanya na kutumia kiasi hicho cha fedha, imetolewa na Waziri wa fedha na Mipango Mwigulu Nchemba, wakati akiwasilisha bungeni mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2023/ 2024.Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zatangaza bajeti zao

Katika hotuba yake Waziri Mwigulu amesema kuwa Sura ya Bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/24 inaonesha kuwa jumla ya shilingi trilioni 44.39 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika huku jumla ya mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 31.38, sawa na asilimia 70.7 ya bajeti yote.

 

Kati ya mapato hayo, mapato yatakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania, yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 26.73 na mapato yasiyo ya kodi (Wizara, Idara, Taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa) yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 4.66.

Misada ya wafadhili

Misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo inatarajiwa kuwa shilingi trilioni 5.47. Aidha, serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 5.44 kutoka soko la ndani ambapo shilingi trilioni 3.54 ni kwa ajili yakulipia hatifungani na dhamana za serikali zinazoiva na kiasi cha shilingi trilioni 1.90 ni kwa ajiliya kugharamia miradi ya maendeleo.

Sikiliza kuhusu bajeti iliyopita: 

Serikali ya Tanzania yaainisha vipaumbele katika bajeti

This browser does not support the audio element.

Miongoni mwa matumaini ya Watanzania katika bajeti hiyo ni pamoja kutatua changamoto za uchumi. Katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/24, maeneo ya vipaumbele ni pamoja na kuendelea kukamilisha miradi ya kielelezo na ile ya kimkakati ikiwemo miradi ya ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR), kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Mwelekeo wa matumizi na mapato ya serikali ya Uganda

Uganda, bajeti iliyowasilishwa inalenga kukusanya kodi zaidi kutoka kwenye bidhaa za msingi ili nchi hiyo iweze kulipa madeni yake ambayo yamendelea kuwa mzigo mkubwa kwa walipaji kodi. Miongoni mwa bidhaa hizo ni vinywaji ikiwemo maji pamoja na nepi za matumizi ya mara moja kwa watoto na wazee.

Kulingana na wizara ya fedha, takribani asilimia 53 ya fedha kwenye makadirio ya matumizi ya mwaka ujao wa fedha zitafadhili kulipa madeni ya nchi. Fedha zilizobaki zitawekezwa katika kulipa mishahara na ujenzi wa miundombinu hususan barabara.

Usalama kupokea fungu kubwa

Bunge la Uganda likiwa katika mojawapo ya kikaoPicha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Sekta ya usalama ndiyo itapokea fungu kubwa huku kilimo na afya vikipata sehemu ndogo zaidi ya mgao wa mapato. Wabunge wa upinzani ambao wengi wamesusia kikao cha bajeti kusomwa wamekosoa jinsi serikali ilivyoipanga bajeti hiyo. Lakini mmoja wa wabunge wa chama tawala cha NRM, Linos Ngombeki ameisifu bajeti hiyo akisema kuwa imezingatia nyanja zote za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Serikali inategemea kuingiza mapato zaidi kutokana na kodi iliyoongezwa kwenye bidhaa muhimu ikiwemo nepi zinazotumiwa mara moja, maji ya chupa na vinywaji vingine. Uganda kuchapua ukuaji uchumi katika mwaka ujao wa kifedhaOngezeko la asilimia kumi ya kodi kwa ada za matumizi ya mitandao ya kijamii limelalamikiwa na vijana wengi. Miongoni mwa matarajio ya wengi ilikuwa kwamba serikali ingezingatia kuwapunguzia wananchi makali ya maisha kutokana na bei za juu za bidhaa kama chakula.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amehutubia kikao hicho kupitia mtandaoni kutokana na kuendelea kusumbuliwa na maambukizo ya virusi vya corona. Hali hii ndiyo imesababisha hata kushindwa kusafiri kwenda Ukraine na Urusi ambako baadhi ya viongozi wa Afrika wameanzisha juhudi za kuupatanisha mzozo kati ya nchi hizo mbili hasimu.Serikali za Tanzania, Kenya na Uganda zawasilisha bajeti kuu

Bajeti ya Kenya

Waziri wa fedha wa Tanzania Mwigulu NchembaPicha: Deo kaji Makomba/DW

Serikali ya Kenya Kwanza imewasilisha bajeti yake ya kwanza bungeni tangu kushika hatamu za uongozi. Takwimu zinaashiria kuwa mfumuko wa bei umepungua kutokea asilimia 9.6 hadi 8 baada ya serikali kuchukua hatua za kuudhibiti tangu Oktoba mwaka uliopit. Miradi ya serikali ya Rais William Ruto itaigharimu nchi shilingi trilioni 3.68 ambayo ni asilimia 22 ya pato la taifa. Wakati huo huo, wabunge wa upinzani walisusia kikao cha leo na kutoka nje wakati bajeti ilipoanza kusomwa.

Bajeti iliyopita: Bajeti kuu Kenya yagonga sh. 3.3 Trilion

Waziri wa Fedha Njuguna Ndungu aliwasili bungeni kusoma makadirio ya bajeti ya mwaka 2023/24 wa fedha. Safari yake ilianzia kwenye majengo ya Wizara ya Fedha aliposindikizwa na maafisa wa ulinzi kwenye barabara ya Harambee katikati ya jiji la Nairobi. Pindi baada ya spika wa bunge la taifa Moses Wetangula alipomkaribisha rasmi jukwaani Waziri Ndungu, wabunge wa upinzani walimzomea na kutoka nje na hatimaye kususia kikao.

Wabunge hao waliongozwa na kiongozi wa upinzani bungeni Opiyo Wandayi. Waziri Ndungu aliendelea kuisoma bajeti chini ya uelekezi wa Spika wa Bunge la taifa Moses Wetangula. Waziri huyo aliweka bayana kuwa serikali itakopa jumla ya shilingi bilioni 718 katika mwaka ujao wa fedha ambazo ni sawa na 4.4% ya pato la taifa na alisisitiza kuwa mpango wa serikali ni kupunguza madeni ya umma.

Sekta ya elimu yapewa fungu kubwa

Sekta ya usalama imetengewa shilingi bilioni 338 za Kenya. Wizara ya elimu imetengewa sehemu kubwa ya bajeti ambayo ni shilingi bilioni 628.6 sawa na asilimia 27.4 ya bajeti yote. Duru zinaeleza kuwa serikali inapanga kupunguza mikopo kutoka shilingi bilioni 849 ilizokadiriwa mwaka wa fedha uliopita wa 2022/23. Rais Ruto ana azma ya kukusanya shilingi bilioni 588.5 kutoka ndani ya nchi huku shilingi bilioni 131.5 zitatokea kwa wafadhili wa kimataifa. Itakumbukwa kuwa Rais Ruto aliahidi kuiondoa Kenya kwenye jukwaa la madeni makubwa kwani huenda ikaiacha nchi pabaya.

Miradi ya serikali itagharimu shilingi trilioni 3.7 za Kenya. Kwenye orodha hii ya matumizi, shilingi bilioni 743 zitatengewa miradi ya maendeleo na gharama za kawaida zitatengewa shilingi trilioni 2.5. Dhamira ya serikali ni kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa kodi.Kenya kukopa shilingi bilioni 2.6 kufadhili oparesheni zake

Bajeti hii inasomwa wakati ambapo mjadala wa muswada wa fedha wa 2023 unaendelea kuzua hisia mseto nje na ndani ya serikali kuu baada ya mjadala mkali hapo jana bungeni.

Ripoti hii imechangiwa na waandishi wa DW: Lubega Emmanuel, Thelma Mwadzya na Deo Makomba.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW