1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Ukiishi na mpenzi bila ndoa marufuku kurithi mali

Thelma Mwadzaya21 Julai 2021

Wabunge nchini Kenya wamewabana wanaoishi kinyumba kurithi mali pindi mpenzi mmoja anapofariki dunia. Kulingana na sheria mume au wake wa ndoa rasmi pekee ndio wanaotambulika kwenye suala la urithi.

Symbolbild Liebespaar, Elfenbeinküste
Picha: picture-alliance/Photononstop

Ijapokuwa sheria ya ndoa inawatambua pia wanaoishi kinyumba kwa muda mrefu, wabunge wamefutilia mbali haki ya walio kwenye hali hiyo kurithi mali mmoja wao anapokufa.

Kwenye kikao cha bunge, viongozi wanaume waliungana na kwa kauli moja walipiga marufuku kitendo cha wanaoishi kinyumba kurithi mali pindi mwenza anapofariki dunia.Wabunge hao walikataa kuridhia mageuzi kwenye mswada wa mirathi wa mwaka 2019 ulionuwia kuwapa haki ya kurithi wenza wanaoishi kinyumba bila ya ndoa.Kimsingi mke au mume ni yule aliyefunga ndoa rasmi kwa mujibu wa sheria na ndiye aliye na haki ya kurithi mali ya atakayefariki. Mbunge wa HomaBay mjini Peter Kaluma na ndiye aliyewasilisha mswada huo kikaoni.

Maharusi nchini KenyaPicha: Getty Images/AFP/S. Maina

Mbunge huyo wa HomaBay Mjini Peter Kaluma alidhamiria kuwasilisha marekebisho yatakayoupa mswada huo wa ndoa makali ya kuwawezesha walioishi kinyumba kwa miaka isiyopungua mitatu kabla ya kifo cha mmoja wao kurithi mali yake.Kimsingi waliojitambulisha kwa familia zao kuwa wanaishi kinyumba japo hawajaozwa rasmi kisheria wangeweza kurithi mali ya mpenzi aliyefariki.Ifahamike kuwa kisheria, kitendo cha kuishi kinyumba kwa muda mrefu kinatambulika hata bila kuozwa rasmi ilimuradi wapenzi hao wanaishi katika mazingira ya ndoa.

Wabunge hao wanaume walishikilia kuwa sharti anayetaka kurithi mali ya aliyefariki dunia aozeshwe rasmi kabla ya kifo cha mwenzake. Kwa mtazamo wa wabunge, marekebisho hayo yalidhamiria kuwapenyeza wapenzi wa kando wa siri ili wanufaike na ndio sababu waliyapinga.

Mswada huo unalenga kufafanua warithi rasmi na halali kadhalika kuwalinda watoto, mke au mume na jamaa zake kwa jumla.Kwa upande mwengine mswada huo una azma ya kuidhibiti idadi ya wanaodai urithi wa marehemu na pia kuwatambua watoto wake hata ikiwa hawakuishi pamoja katika uhai wake.Jee wakenya wana mtazamo upi kuhusu mswada huo? Baadhi walikuwa na haya ya kusema.

Orodha ya watakaorithi mali ya marehemu inajumuisha pia wazazi,wajukuu, watoto wa kambo na wa kuwalea ambao hakuwazaa, nduguze na wote waliosimamiwa naye kabla kifo chake.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW