Kenya: Upasuaji wa kufunga mirija ya uzazi waongezeka
4 Oktoba 2023Upangaji uzazi miongoni mwa wanaume ni hoja ambayo haizungumziwi sana katika majukwaa ya kijamii hadi kwenye miungano ya mahusiano ya kimapenzi hasa ndoa, huku baadhi ya sababu zikihusisha taasubi za kiume au kujiona kuwa muhimu, dini, taarifa stahiki miongoni mwa mengine.
Mada hii tangu jadi imekuwa ikiwahusisha wanawake ambao wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za kupanga uzazi kupitia njia mbalimbali kama vile kumeza vidonge, sindano, kuweka kitanzi sehemu ya uzazi, au vijiti sehemu ya mkono.
Kijana Imran Mansoor ni mmoja wa wanaopinga kabisa matumizi ya mifumo ya kupanga uzazi miongoni mwa wanaume.
"Hili ni suala ambalo nalikataa. Katika misingi binafsi ya kidini."
Katika mahojiano na DW, Ali Bakari ambaye ni mwanaharakati wa masuala ya kijamii kutoka Likoni, pwani ya Kenya ananieleza kuwa, kupanga uzazi miongoni mwa wanaume ni hatua inayostahili kuhamasishwa katika jamii ila ni muhimu kuzingatia kuwa baadhi ya jamii zinazofungama na dini, hazikubaliani na mpango huo.
Anasema baadhi ya wanaume wanakosa kushiriki zoezi hili kutokana na hofu ambayo inaweza kudhibitiwa kupitia uhamasishaji.
Soma pia: Je wanaume huchukulia vipi suala la upangaji uzazi?
Kauli sawi na hii inatolewa na Maimuna Mwinyi, mtaalamu wa masuala ya kijamii katika jimbo la Nakuru, Kenya, ambaye anahimiza usirikiano baina ya walio na mahusiano kutoa uamuzi wa pamoja endapo mume atafanyiwa upasuaji huu wa kufunga mirija ya uzazi, "Suala la kupanga uzazi halipaswi kuachiwa wanawake pekee."
Mhudumu wa afya katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Jaramogi Oginga Odinga, Victor Okong'o anasema kupanga uzazi wa wanaume kwa kufunga mirija ya uzazi ni hatua salama ambayo pia ina faida za kiafya na kabla ya kuchukua hatua hii ni sharti mhusika awe amefanya uamuzi na hivyo anapendekeza uhamasishaji zaidi kuendeshwa katika jamii, "Utasalia kawaida, na hata wewe mwenyewe utajiweka salama."
Kuhusu gharama ya upasuaji huu kuwa juu, serikali nchini Kenya inaendelea kuhakikisha huduma hii inaendeshwa bila malipo katika hospitali za umma, kama anavyoelezea afisa wa afya Beth Onyango, "Wanaume wajitokeze kushiriki zoezi hili maana lina manufaa."
Ili mhusika aweze kufanyiwa upasuaji huu wa mirija inayobeba mbegu za kiume kwa lengo la kuzuia mimba kabisa nchini Kenya, ni sharti mwanaume asaini makubaliano ya kumruhusu mhudumu wa afya kufanya upasuaji huo.