1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: Vikao vya bunge vyaanza tena

Thelma Mwadzaya29 Novemba 2017

Bunge la kitaifa nchini Kenya limerejea vikaoni baada ya mapumziko yaliyoupisha uchaguzi mpya wa mwezi wa Oktoba.Agenda kuu ni kuteua kamati itakayowapiga msasa mawaziri wapya watakaochaguliwa na Rais Uhuru Kenyatta

Nairobi Kenia Abgeordnete Parlament Debatte Sicherheitsgesetz 18.12.2014
Picha: Reuters/T. Mukoya

Bunge la kitaifa nchini Kenya limerejea vikaoni baada ya mapumziko yaliyoupisha uchaguzi mpya wa mwezi wa Oktoba.Agenda kuu ni kuteua kamati itakayowapiga msasa mawaziri wapya watakaochaguliwa na Rais Uhuru Kenyatta. Wakati huohuo wanasiasa wa vyama vya muungano wa NASA hatimaye wamewasilisha orodha ya majina ya washirika wao wa kamati za bunge za utendaji. Hata hivyo wabunge wanaotokea eneo la pwani wa NASA wanatishia kukwamisha shughuli za chama kwa madai ya kutengwa. Rais Uhuru anakabiliana na kibarua kigumu kuinganisha nchi kwasababu ya tofauti za kisiasa zilizoko.

Kikao cha bunge kilianza rasmi asubuhi baada ya mapumziko ya wiki tatu yaliyoupisha uchaguzi mpya wa rais. Rais Uhuru Kenyatta aliapishwa jana uwanjani kasarani jijini Nairobi kufuatia kipindi cha mvutano wa kisiasa na wenzake wa upinzani wa NASA. Wabunge hao walikuwa na ajenda nzito ya kuiteua kamati itakayowapiga msasa mawaziri wapya watakaoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Kibarua cha kuwa na baraza la mawaziri lenye sura ya kitaifa

Rais Kenyatta ana kibarua kigumu cha kuhakikisha kuwa baraza lake jipya linapata sura ya kitaifa pasina kuwasogeza karibu wafuasi wa upinzani waliomuunga mkono katika uchaguzi mkuu uliopita. Kadhalika huu ndio wakati wa kuanza kuandaa mikakati ya kuwajumuisha washirika wapya kabla uchaguzi mkuu wa 2022.

Tetesi zimezagaa kuwa nusu ya idadi ya mawaziri waliohudumu katika serikali iliyopita huenda wakatimuliwa kwa sababu ya utendaji wao. Ifahamike kuwa katiba inampa rais uwezo wa kuwateua mawaziri wasiopungua 14 na wasiozidi 22. Kulingana na kigezo hiki Rais Uhuru analazimika kuwabadilishia nyadhifa mawaziri walioko, kuzigawa baadhi ya wizara na kujaza nafasi zote 22 ili kuonekana kuwa na taswira ya kitaifa na kuwashirikisha waliofanikisha harakati za chama cha Jubilee katika awamu mbili za uchaguzi zilizofanyika. Kwa sasa baraza lina wizara 20 na mawaziri 19.

Wabunge wa NASA kutoka Pwani wahisi kutengwa

Wakati huo huo mapema bungeni kulizuka sokomoko baada ya wabunge wanaotokea eneo la pwani wa vyama vya muungano wa upinzani wa NASA kutishia kukwamisha shughuli za chama kwa madai ya kutengwa kwenye uteuzi wa washirika wa kamati za bunge.

Wabunge wa upinzani wametishia kutoshiriki kwenye mipango yoyote ya kuunda kamati za utendaji bungeni Picha: Reuters/T. Mukoya

Kiongozi wa wachache bungeni aliyeteuliwa ni Mbunge wa Suba Kusini John Mbadi na kiranja ni Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed.Wawili hao ni wa chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga.Manaibu wao ni Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa wa Ford Kenya na Robert Mbui wa chama cha Wiper anayetokea eneo bunge la Kathiani. Kwa sasa tayari upande wa upinzani wa NASA umewasilisha kwa spika wa bunge la taifa Justin Muturi orodha ya majina ya wawakilishi wake katika kamati za bunge.

Spika wa Bunge la kitaifa Justin Muturi alikiri kuwa ameipokea orosha ya wabunge wa upinzani kushiriki kwenye kamati za bunge na sasa inasubiri ridhaa yake.Hata hivyo upinzani bado haujafikia mwafaka kuhusu wanachama watakaowawakilisha kwenye kamati ya Uwekezaji wa Umma na Uhasibu wa umma .Mchakato huo ulisuasua kwasababu ya mivutano kati ya vyama vinanvyounda muungano wa NASA vya ODM, Wiper,ANC na Ford Kenya mintarafu jinsi ya kugawanya nafasi hizo.

Kadhalika wabunge wa upinzani walikuwa wanatishia kutoshiriki kwenye mipango yoyote ya kuunda kamati za utendaji bungeni kwani wanashikilia hawaitambui serikali inayoongozwa na Jubilee. Je ipi athari ya wabunge wa upinzani kususia shughuli za bunge? Hilo ndilo suali nililomuuliza Joy Mdivo, mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Sheria cha Afrika Mashariki,EACLJ.

Bunge la 12 lilianza kazi rasmi mwezi wa Septemba ila hakuna kamati ya utendaji iliyoundwa kwasababu ya tofauti za kisiasa zilizokuwako. Kibarua kinachomsubiri Rais Uhuru Kenyatta ni kuwaunganisha wakenya wakati mpasuko wa kisiasa bado unashuhudiwa kwani wafuasi wa upinzani wanashikilia kiongozi wao Raila Odinga ataapishwa tarehe 12 mwezi ujao wa Disemba ambayo ni sikukuu ya kitaifa ya Jamhuri.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya, DW.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW