Kenya: William Ruto atishia kukihama chama tawala
16 Aprili 2021Katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini Kenya, Ruto aliyeonekana kuzidiwa na jazba, alisikitishwa na jinsi wabunge wanaoegemea upande wake walivyotimuliwa kwenye nafasi za uwenyeviti wa kamati za bunge na baadhi ya mawaziri pia kuondolewa na kushtakiwa kwa kuhusika kwenye ufisadi.
Seneta wa Elgeyo-Marakwet, Kipchumba Murkomen, aliondolewa kwenye wadhfa wa kiongozi wa wengi katika bunge la seneti huku mwenzake wa Nakuru Susan Kihika, akiondolewa kuwa kiranja. Hata hivyo Ruto amesisitiza kuwa bado anamheshimu rais Uhuru Kenyatta.
"Ningali na matumaini kwamba chama cha Jubilee kitabadilika na kurejea kwenye maono ya kwanza, lakini hilo lisipofanyika, lazima tuwe na mikakati, sisi tuna bahati kwa sababu tuna chama cha UDA. Jubilee ikiendelea kutuvuruga, lazima ufikirie,” alisema William Ruto
soma zaidi: Mvutano wandelea kati ya washirika wa Ruto na serikali
Mapema mwaka huu, Chama cha Jubilee kilipendekeza kutimuliwa kwa maseneta maalum wanaogemea upande wa Ruto. Mahusiano kati yake na rais Uhuru Kenyatta yanaonekana kuingia doa baada ya Ruto kusema atagombea kiti cha urais, kwenye uchaguzi mkuu ujao, ama rais amuunge mkono au asimuunge.
Kwanini rais Kenyatta na naibu wake William Ruto hawaelewani?
Tangu Rais Kenyatta na kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement Raila Odinga kufanya mwafaka tarehe tisa Machi, mwaka 2018, mahusiano kati ya Kenyatta na Ruto yamekuwa yakididimia.
Mara kadhaa Ruto amekosa kualikwa kwenye mikutano ya baraza la mawaziri na shughuli nyingine za serikali kama vile kuhusishwa kwenye kamati ya kukabiliana na virusi vya Korona.
Felix Ochieng ni mtaalamu wa masuala ya siasa anasema uhusiano kati ya rais na makamu wake ulikuwa wa nazi kukutania chunguni.
soma zaidi: Wafuasi wa Ruto wahoji ushindi mkubwa wa BBI kwenye kaunti
Hata hivyo Ruto alikosa kumlimbikizia lawama bosi wake ambaye pia ni rais akisema kuwa siku zote kiongozi yu sahihi hata baada ya Rais kumchagua Waziri wa Usalama wa Taifa Dokta Fred Matiangi kuchukua baadhi ya majukumu yake.
Kuhusu suala la Rais kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu ujao, Ruto alijitenga na matamshi hayo akisema kuwa, ni rais mwenyewe aliyeyasema, lakini akaongeza kuwa, rais ana haki ya kubadilisha msimamo wake.
Hii ndio mara ya kwanza tangu misuagano ndani ya chama cha Jubilee kuanza, makamu wa rais amejitokeza wazi na kuelezea nia ya kukihama chama cha hicho. Wapambe wa siasa wa Ruto sasa wanapanga jinsi ya kushirikiana na kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye wataalam wanasema anahadaiwa na Rais.
Mwandishi: Shisia Wasilwa, DW Nairobi