1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaamuru kufungwa kwa mabweni ya shule 348

5 Desemba 2024

Wizara ya elimu imeamuru kufungwa kwa mabweni ya shule 348 nchini Kenya. Tathmini ya kina iliyofanywa Septemba na Oktoba 2024 ilibaini kuwa shule hizo zilishindwa kuhakikisha viwango muhimu vya usalama kwa wanafunzi.

Kenya | Nyeri | Moto | Hillside Endarasha Primary School
Wazazi wakikusanyika nje ya shule ya kaunti ya Nyeri Hillside Endarasha Academy katika kaunti ya Nyeri baada ya moto kuzuka na kuua wanafunzi 17.Picha: Simon Maina/AFP

Kupitia taarifa rasmi, katibu mkuu katika wizara ya elimu Belio Kipsang amesema kuwa shule za msingi 348 hazijakidhi viwango vya shule za bweni na hivyo kuziamuru kufungwa mabweni yao mara moja.

Kipsang alisema shule hizo hazijakidhi viwango vya usalama katika utafiti wa kina uliofanywa kati ya Septemba na Oktoba 2024.

Zoezi la tathmini ya kubainisha uzingatiaji wa viwango vya usalama kwa shule zote za bweni nchini lilifanyika katika miezi ya Septemba na Oktoba 2024.

Nairobi inaongoza kwa shule 40 ambazo hazijakidhi viwango hitajika, ikifuatiwa na Kericho yenye shule 26, Uasin Gishu yenye shule 19, Nandi yenye shule 15, na Kiambu na Kisii zilikiwa na shule 13 kila moja.

Wanafunzi 21 wafariki katika mkasa wa moto Nyeri

Miili ya wanafunzi waliofariki baada ya kutokea moto katika shule ya Hillside Endarasha, kaunti ya Nyeri. Picha: Edwin Walta/REUTERS

Haya yanajiri baada ya mkasa wa moto katika shule ya bweni ya Hillside Endarasha katika kaunti ya Nyeri ambao ulisababisha vifo vya wavulana 21 wenye umri wa kati ya miaka 9 hadi 14 usiku wa tarehe 5 Septemba.

Hii ilisababisha serikali kuchukua hatua kuhakikisha usalama wa watoto wakiwa shuleni kama anavyoeleza Waziri wa elimu wa Kenya Julius Ogamba.

"Labda kama nchi imefikia wakati tunapohitaji kuzingatia masharti na kanuni hizo na kujua kama ni wakati wa sisi kupiga hatua zaidi na kuzipitisha kuwa sheria ili kuwe na adhabu zitakazoambatana nazo kwa yeyote atakayezikiuka, kwa sababu hatuwezi kuendelea hivi kama nchi."

Soma pia: Kenya: Mikasa ya moto mashuleni yachochea hofu kwa wanafunzi

Wakati wa zoezi la tathmini, wasiwasi mkubwa ulionyeshwa kwenye masuala ya usalama wa mabweni, usafi wa mazingira, usimamizi wa vifaa vya moto, na ustawi wa jumla wa wanafunzi.

Wizara ya elimu imewaamuru wakurugenzi wa elimu wa Mikoa na Kata kuhakikisha sehemu ya bweni katika shule hizi bado imefungwa kwani zinakiuka viwango vya usalama kuambatana na mwongozo wa shule wa mwaka 2008. Wakuu hao wametakiwa kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa kuanzia Januari 2025, kwamba wanapaswa kufanya kazi kama shule za kutwa.

Usalama wa wanafunzi katika shule za bweni Kenya

02:37

This browser does not support the video element.

Mwongozo huo ambao ulitengenezwa mwaka 2008 unaonyesha hatua muhimu za usalama, ikiwa ni pamoja na miundombinu sahihi, itifaki za dharura, na majukumu ya wasimamizi wa shule katika kuhakikisha usalama wa wanafunzi.

Mfumo wa elimu nchini Kenya umekuwa ukikabiliwa na changamoto nyingi, kuanzia ukosefu wa mbinu muafaka za ufadhili, ukosefu wa usawa, hali duni ya miundombinu, ukosefu wa utekelezaji wa sera na matukio ya mikasa kama vile ya moto shuleni.

Wakati wa uzinduzi wa mwongozo kuhusu mfumo wa viwango vya ubora wa elimu, ripoti ya mashirika ya kijamii chini ya kundi la Elimu Bora ilipendekeza kwamba, ili kurekebisha kikamilifu mfumo wa elimu, serikali inapaswa kuanzisha hazina ya kitaifa ya elimu, sera ya kitaifa kuhusu elimu ,utekelezaji kamili wa elimu ya msingi bila malipo na ya lazima, kuanzisha mfumo wa uwazi na uwajibikaji.

Soma pia: Kenya yajitahidi kuboresha miundombinu ya walemavu

Boaz Waruku, mwakilishi wa kundi hilo amesema "Katika kwenda mbele mchakato wowote wa mageuzi utafinikiwa iwapo wadau wote watajumuishwa na kushiriki kikamilifu katika michakato hiyo. Na wanapofanya hivyo pia tunasisitiza kwamba kanuni ambayo inapaswa kuongoza utekelezaji wa mchakato au ripoti yoyote inapaswa kwanza kabisa kutegemea kanuni ya haki za binadamu."

Umesalia mwezi mmoja tu kabla ya shule kufunguliwa tena mwezi Januari. Wazazi walio na watoto kwenye shule za msingi za bweni wameshauriwa kuandaa mipango mbadala kabla ya muhula wa shule wa mwaka 2025 huku serikali ikitoa kalenda ya shule ya mwaka ujao.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW