1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaanza kusafirisha mafuta ghafi

Angela Mdungu
26 Agosti 2019

Kwa mara ya kwanza Kenya imesafirisha mafuta ghafi kwenda nchini Malaysia. Kiasi cha mapipa laki mbili ya mafuta ghafi yameanza kusafirishwa kwa meli hii leo kutoka bandarini Mombasa.

Kenia Hafen in Mombasa
Picha: Imago Images/Xinhua/M. Cazeiya

Akiongoza hafla ya kuanza kwa safari za meli kupeleka mafuta hayo katika soko la Kimataifa, rais Uhuru Kenyattaa amesema mafanikio hayo ni ya kihistoria kwa watu wa Kenya tangu taifa hilo lilipoanza harakati za kutafuta mafuta na gesi mwaka 1937. Rais Uhuru ameeleza kwamba biashara ya mafuta ni mwanzo mpya kwa Kenya na Afrika ya Mashariki.

Vile vile ameeleza kwamba kwa sasa mabadiliko yaliyofanyika katika sekta ya usafiri wa majini kupitia kampuni ya Mediterenia, Kenya itaweza kufanya biashara na zaidi ya bandari mia tano duniani.

Rais Kenyatta amesema kuanza kusafirishwa kwa mafuta haya ghafi kama majaribio katika soko la kimataifa ni jambo linalotia moyo na kuhakikisha kwamba taifa la Kenya litaweza kutimiza azma yake ya kuwa taifa lililo na rasilimali ya mafuta na gesi.

Mafuta hayo ghafi yanayochimbwa katika eneo la Lokichar kaunti ya Turkana, yamekuwa yakivunwa tangu mwaka jana na kusafirishwa kwa malori hadi bandarini Mombasa. Rais Uhuru ameeleza kwamba serikali yake imeweka mikakati ya kuhakikisha wakenya wote wanafaidika kutokana na pato la mafuta hayo.

Katika hafla hiyo gavana wa Mombasa, Hassan Ali Joho amemtaka rais Kenyatta kufufua kiwanda cha kusafisha mafuta ghafi kilichoko katika eneo bunge la Changamwe karibu na bandari ya Mombasa kilichofungwa miaka mingi nyuma. Vile vile gavana Joho ameitaka serikali kuwekeza zaidi kiviwanda mjini Mombasa ili mafuta hayo yaweze kutumiwa kutengeneza bidhaa mbali mbali zitakazouzwa ng`ambo pamoja na mafuta yaliosafishwa.

Kampuni ya Tullow iligundua uwepo wa mafuta katika ardhi ya Lokichar kaunti ya Turkana mwaka 2012.

Mwandishi: Faiz Musa, DW Mombasa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW