Kenya yaashiria kuunga mkono kuahirishwa kwa AFCON 2027
13 Februari 2026
Kauli hiyo imetolewa na Nicholas Musonye, mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Ndani ya Kenya, katika mahojiano na shirika la habari la AFP.
Gazeti la The Guardian la Uingereza liliripoti kwamba mashindano hayo yanaweza kusogezwa hadi mwaka 2028, likitoa sababu mbili kuu: nchi mwenyeji—Kenya, Uganda na Tanzania—bado hazijawa tayari kikamilifu kuandaa mashindano hayo makubwa na ratiba ya uchaguzi wa Kenya mwaka 2027, ambayo huenda ikaleta mazingira yasiyo tulivu kwa maandalizi na usalama wa mashindano.
Kwa sasa, timu ya ukaguzi kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) iko nchini Tanzania na inatarajiwa kufanya mkutano muhimu leo Ijumaa kujadili hatua zilizopigwa na changamoto zilizopo katika maandalizi ya AFCON 2027.
Rais wa CAF, Patrice Motsepe, hapo awali alionyesha matumaini kwamba AFCON 2027 itafanyika kama ilivyopangwa, akisisitiza dhamira ya shirikisho hilo kuona mashindano hayo yakifanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza katika historia.
Hata hivyo, kauli ya Musonye imeleta mtazamo tofauti kutoka upande wa Kenya. Akihojiwa na AFP, Musonye alisema kuwa kuahirisha mashindano hayo hadi mwaka 2028 "ingekuwa jambo jema kwa Kenya," akibainisha kuwa nchi hiyo itakuwa katika kipindi cha maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Agosti 2027—kipindi ambacho mara nyingi huambatana na mvutano wa kisiasa.