1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yafanya tathimini ya hali baada ya Maandamano

26 Juni 2024

Kenya inafanya tathmini ya hali baada ya siku nzima ya vurugu na maandamano yaliyoigubika miji kadhaa kote nchini humo. Miili isiyopungua 7 inaripotiwa kufikishwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti mjini Nairobi.

Kenia | Maandamano Nairobi | Ofisi ya Gavana yatiwa moto
Kenya yafanya tathimini ya hali baada ya MaandamanoPicha: Brian Inganga/AP Photo/picture alliance

Duru zinaeleza kwamba maiti zisizopungua 7 zilifikishwa kwenye chumba cha City jijini Nairobi.Kwa mujibu wa maafisa wa chumba hicho cha hifadhi, maiti hizo zilikuwa na majeraha ya risasi na moja ilionesha dalili za kukabwa koo.

Kulingana na taratibu,maiti zinazopatikana kwenye mazingira ya vurugu na maandamano sharti zifikishwe kwenye chumba cha maiti cha serikali ili kutambuliwa na kukaguliwa. Wakati huohuo, wakaazi wa mtaa wa Githurai wanadai wengi walijeruhiwa kwenye mapambano na maafisa wa usalama ila polisi bado hawajathibitisha taarifa hizo.

Waandamanaji Kenya waapa kurudi tena barabarani

Usiku wa kuamkia leo (26.06.2024) Rais William Ruto akilihutubia taifa alisisitiza kuwa vitendo vya Jumanne ni sawa na uhaini na serikali haitosita kuchukua hatua. Viongozi wa upinzani wanasisitiza kuwa suluhu iko kwenye katiba. 

Demokrasia lazima izingatiwe katika maandamano

Waandamanaji waliojawa na hasira wakibeba mabango ya kupinga mswada wa fedha 2024 katika maandamano yaliyofanyika NairobiPicha: Luis Tato/AFP

Kufuatia matukio hayo na vurumai, mabalozi wa nchi za kigeni wameelezea wasiwasi wao ukizingatia maandamano ya kupinga mswada wa fedha wa 2024. Kwenye taarifa yao ya pamoja, wanadiplomasia hao walisisitiza kuwa ijapokuwa ni haki ya wakenya kuandamana, demokrasia lazima izingatiwe.

Kiongozi wa upinzani wa ODM Raila Odinga amemrai rais William Ruto kusubiri kabla ya kutia saini mswada wa fedha wa 2024 unaozua utata hadi pale manunguniko ya wakenya yatakapofanyiwa kazi. 

Waandamanaji wavamia jengo la bunge Kenya

Kwa upande wake, rais mstaafu Uhuru Kenyatta amemtolea wito mrithi wake William Ruto kujizuwia na kukumbatia mazungumzo. Javas Bigamba mchambuzi wa masuala ya siasa na uongozi amesema serikali haina budi ila kuwalinda wote.

Ifahamike kuwa macho yote yanamuangazia rais Ruto ambaye ndiye mwenye uwezo wa kuurejesha mswada huo wa utata ufanyiwe kazi upya au autie saini na uwe sheria. Wakenya wanaendelea kusisitiza kuwa sauti zao ni lazima zisikike.  

Thelma Mwadzaya 
DW Nairobi. 
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW