1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yagawanywa na maamuzi ya ICC

24 Januari 2012

Maoni tofauti yanaendelea kutolewa nchini Kenya siku moja baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kutoa uamuzi wa kuthibitisha mashtaka dhidi ya washukiwa wanne kati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Rais Mwai Kibaki wa Kenya.
Rais Mwai Kibaki wa Kenya.Picha: AP Photo

Uamuzi huo umewafadhaisha wengi akiwamo Makamu wa Rais ,Stephen Kalonzo Musyoka. “Mimi binafsi nimesikitishwa na uamuzi huo wa kuthibitishwa kwa mashtaka.”

Hata hivyo, kuna wale wanaoamini kuwa haki imetendeka kwa walioachiliwa huru, kama vile waziri wa zamani wa sheria nchini Kenya, Kiraitu Murungi, ambaye anasema hata kwa Henry Kosgei na Meja Jenerali Mstaafu Hussein Ali nako haki imetendeka kwa kutoonekana na mashitaka ya kujibu.

Baada ya uamuzi huo wa Mahakama ya ICC kutolewa, Rais Mwai Kibaki alikuwa mwepesi kusema kwamba sasa Kenya ina idara ya mahakama ambayo imefanyiwa marekebisho na ofisi huru ya kiongozi wa mashtaka ya umma.

"Nimemuagiza Mkuu wa Sheria kubuni kundi la wataalam wa kisheria kuchunguza uamuzi huo na kutoa ushauri juu ya hatua ya kuchukua.” Alisema Kibaki.

Bila shaka ni pigo kubwa kwa washtakiwa wawili, Mbunge wa Eldoret Kaskazini William Rutto na Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta ambao wametangaza nia yao ya kuwania wadhifa wa Urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Makamo wa Rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka.Picha: AP Photo

“Vile nilivyosoma na kuielewa katiba na kufuatia ushauri niliopewa na mawakili wangu ni thibitisho kamili kwamba niko kwenye kinyanganyiro na nawaambia washindani wangu kwamba tutakutana kwa debe”. Amesema Ruto.

Washtakiwa hao wanne wakiwa ni pamoja na mtangazaji wa redio, Joshua Sang, na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Balozi Farancis Muthaura, wanazo siku nne kukata rufaa au la wasubiri kesi ianze rasmi.

Mwendesha Mashtaka mkuu Louis Moreno Ocampo anatarajiwa kutoa taarifa yake kwa vyombo vya habari mchana wa leo moja kwa moja kupitia runinga kutoka makao makuu ya ICC huko The Hague Uholanzi.

Ripoti: Alfred Kiti/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW