Kenya yahamishia uchukuzi wa mizigo Naivasha
2 Juni 2020Kulingana na waziri wa Uchukuzi wa Kenya James Macharia, amri hii inaambatana na agizo la viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki la kuzuwia virusi vya corona kusambaa wakati madereva wa malori wanasafirisha bidhaa.
Waziri Macharia anasisitiza kuwa manufaa ni mengi zaidi kwa wafanyabiashara hao kupokea mizigo yao kutokea Naivasa badala ya bandarini Mombasa.
Bandari ya nchi ya kavu ya Naivasha inasadikika kuwa na vifaa vinavyohitajika kama vilivyoko Mombasa kurahisisha shughuli ya kusafirisha mizigo.
Kadhalika mbali ya kuwako nafasi ya kutengeza afisi za muda kwa kampuni husika, makasha matupu yatasafirishwa moja kwa moja hadi Mombasa bila malipo ya ziada.
Kimsingi hakuna malipo ya ziada baada ya kupokea mizigo kwenye bandari ya nchi kavu ya Naivasha na kwa sasa wafanyabishara hawatozwi chochote kuhifadhi makasha yao kwenye mabohari hayo.
Wadau wataka wateja wapewe chaguo
Hata hivyo wafanyabishara wa kusafirisha mizigo kwa malori ya safari ndefu wana mtazamo tofauti. Dennis Ombok, Afisa mkuu mtendaji wa chama cha wafanyabiashara wa kusafirisha mizigo nchini Kenya, anasema SGR ni njia moja ya usafiri na barabara ni nyengine. "Tunachokiomba kwa serikali ni kuwe na usawa na haki ili mteja aweze kuamua mfumo wa usafiri anaoutaka."
Takwimu za Wizara ya Uchukuzi ya Kenya, zinaashiria kuwa mfanyabiashara atahitaji kati ya dola 1,930 na 2180 kusafirisha kasha la futi 20 na 40. Waziri wa uchukuzi anashikilia kuwa ipo mipango ya kuifufua reli inayoziunganisha Mombasa na Malaba iliyoko mpakani. Hata hivyo hatua hii imepingwa na washika dau wa eneo la Afrika Mashariki.
Wiki iliyopita Uganda iliirai Kenya kulitathmini upya agizo la kupokea makasha kutokea Naivasha bila mafanikio. Msimamo wa Uganda unaungwa mkono na washika dau wa Kongo, Rwanda,na Sudan Kusini.
Viongozi wa pwani wana hisia mseto na kusisitiza kuwa wakazi watapoteza nafasi muhimu ya kuchuma pato la kila siku. "Hali ya uchumi au hali ya biashara katika kaunti ya Mombasa imekuwa mbaya sana. Na tegemeo kubwa kabisa la watu wa pwani ni port (bandari).Na ikiwa mizigo haitachukuliwa na magari pale port italeta shida sana," amsema Issa Boy Juma, seneta wa Kaunti ya Kwale.
Hii leo Waziri wa Uchukuzi wa Kenya James Macharia anatazamiwa kufika bungeni kuelezea hatua hii mpya ambayo imezua mitizamo tofauti. Ili kufanikisha mipango hii, shehena ya kwanza ya makasha 200 ya futi 20 ilihamishwa kutokea Mombasa hadi Naivasha kwa reli tarehe 7 mwezi wa Mei.