Kenya yahitimisha siku ya tatu ya maandamano
21 Julai 2023Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yanawakashifu maafisa wa polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi kuwakabili waandamanaji. Nayo serikali ya Kenya Kwanza imewatetea polisi kwa kuwajibika. Rais William Ruto amsititiza kuwa wahalifu hawana nafasi katika jamii.
Soma pia: Polisi wa Kenya walizuiwa kuripoti vifo wakati wa maandamano
Viongozi wa upinzani wa Azimio la Umoja wanajiandaa kwa hatua mpya baada ya maandamano ya siku tatu kufikia kikomo hii leo. Hata hivyo shughuli katika maeneo ya nchi zilionekana kuendelea tofauti na ilivyokuwa katika siku ya kwanza na ya pili ya maandamano. Kufikia sasa bado vinara wake hawajaonekana hadharani. Duru zinaeleza kuwa kiongozi wa Wiper Demokratik Kalonzo Musyoka alilazimika kubaki nyumbani kwake kwani maafisa wa polisi wamekuwa wakiyazingira makaazi yake tangu Jumanne.
Raila Odinga aliyezungumza na kituo cha habari cha NTV alibainisha kuwa anaugua mafua makali hivyo basi analazimika kusalia ndani.
Akizungumza na waandishi wa habari, kiongozi wa upinzani bungeni Opiyo Wandayi aliwasifu wakenya kwa kujitokeza kuandamana na katika saa chache zijazo watatangaza muelekeo wa kufuata wiki ijayo.
Soma pia: Zaidi ya waandamanaji 300 washikiliwa na polisi nchini Kenya
Raila pia amekanusha kufanya mazungumzo na mabalozi wa kigeni kuhusu maandamano.
Mlinzi wa Raila kufikishwa mahakamani
Huku hayo yakijiri, jaji Lawrence Mugambi amemuamuru Inspekta mkuu wa polisi Japheth Koome amfikishe mahakamani mara moja mlinzi wa kinara wa ODM Raila Odinga. Maurice Ogeta alikamatwa na kuzuiliwa na watu wanaosadikika kuwa polisi, yalipoanza maandamano ya wiki hii.
Familia yake pia inashinikiza mpendwa wao aachiliwe la sivyo waanze mchakato wa kisheria. Kadhalika, familia ya kiongozi wa zamani wa kundi haramu la Mungiki Maina Njenga inaishinikiza serikali kumuachilia huru baada ya yeye kukamatwa wiki hii nyumbani kwake Matasia pamoja na nduguye.
Akizungumza kwenye mahakama ya Milimani, msemaji wa familia Murugaru Kamiti alisisitiza kuwa wanakiuka sheria.
Kwa upande wao, mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International, Human Rights Watch na tume ya kutetea haki za binadamu ya Kenya, KHRC, wamwanyoshea kidole cha lawama maafisa wa polisi kwa mauaji, misako na kuwajeruhi waandamanaji walipotumia nguvu kupita kiasi. Ndindi Nyoro ni mbunge wa Kiharu kutoka chama tawala cha UDA na anashikilia kuwa polisi waliwajibika.
Viongozi wa kidini wanausisitizia umuhimu wa kurejea kwenye meza ya mazungumzo kusaka suluhu.Yote hayo yakiendelea, rais William Ruto ameendelea na ziara za kuzindua miradi ya maendeleo kwenye kaunti.Akihutubu Muranga, rais William Ruto alisisitiza kuwa wahalifu hawana nafasi katika jamii.
Takwimu za chama cha wafanyabiashara wa uzalishaji KAM zinaashiria kuwa sekta ya uchumi inapoteza shilingi bilioni 2.86 kila siku kwenye maandamano.
Tazama pia: