Kenya yajiandaa kwa uchaguzi
7 Agosti 2017Wakenya milioni 19 wanatarajia kushiriki kwenye uchaguzi wa kihistoria hapo kesho, huku matayarisho yote yakikamilika. Kiongozi wa chama tawala cha Jubilee, Rais Uhuru Kenyatta, anakutana tena na hasimu wake wa kisiasa, Raila Odinga, wa muungano mkuu wa upinzani, NASA, kwenye kinyang'anyiro kinachotazamiwa kuwa cha vuta-nikuvute baina ya wawili hao, licha kuwepo wagombea wengine saba wa urais.
Siku ya mwisho kabla ya uchaguzi
Zikiwa zimesalia saa za kuhesabu, Wakenya wanasubiri kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano siku ya Jumanne. Uchaguzi huu unaowagharimu walipakodi wa Kenya shilingi bilioni 49 unaonekana kuwa ghali zaidi ukilinganishwa na chaguzi katika mataifa jirani.
Zaidi ya wagombea 1,000 watachaguliwa na Wakenya milioni 19 kwenye nafasi za urais, ugavana, useneta, ubunge, uwakilishi wa kinamama na wa kaunti. Kuna vituo elfu 40,883 vya kupigia kura vitakavyolindwa na maafisa 150,000 wa idara za usalama. Zaidi ya waangalizi 9,000 wa kitaifa na wa kigeni wameidhinishwa kuangalia uchaguzi huu.
Wito wa amani
Jijini Nairobi hali ni tulivu huku shughuli za kawaida zikipungua. Hakuna misongamano ya magari na kelele ambazo huhanikiza jiji hili na baadhi ya maduka yamefungwa.
Rais Uhuru Kenyatta, ambaye alikamilisha kampeni zake katika mji wa Nakuru juzi Jumamosi, aliwaomba Wakenya wapige kura kwa amani, huku kinara wa upinzani Raila Odinga aliyekamilisha kampeni zake katika Bustani ya Uhuru jijini Nairobi, akiwataka wafuasi wake wajitokeze kwa wingi kupiga kura. Huku Rais Kenyatta akiomba ridhaa ya kuongoza ya kipindi kingine cha miaka mitano, Odinga anaona wakati huu ataibuka mshindi, kwani ameziba mianya mingi ambayo ilikuwa inavuja kwenye chaguzi zilizopita.
Ushindani mkali kati ya Uhuru na Raila
Kura ya maoni iliyofanywa mwezi Januari ilimuweka Rais Kenyatta mbele kwa asilimia 47 dhidi ya Odinga aliyekuwa na asilimia 30. Hata hivyo, juma lililopita kwenye utafiti mwingine, Odinga alikuwa anaongoza kwa asilimia 47 dhidi Kenyatta aliyekuwa na asilimia 46. Wachambuzi wa masuala ya siasa wakisema kuwa uamuzi wa upinzani kutosambaratika hadi sasa umechangia kuchupa kwa Odinga kwenye utafiti huo.
Taasisi ambazo zinahusika kwenye uchaguzi huu, zimetoa hakikisho kuwa ziko tayari kuendesha uchaguzi huru wa haki na wa kuaminika. Macho yote yatakuwa yakielekezwa kwenye tume inayosimamia uchaguzi huu, IEBC, idara ya usalama na idara ya mahakama.
Tangazo la IEBC hapo jana kuwa matokeo kwenye vituo 11,000 vya kupigia kura hayatapeperushwa kwa njia ya elektroniki yanatamausha, kwani maeneo mengi yaliyotajwa yamo kwenye miji.
Hata hivyo, matumaini ya Wakenya ni kuwa uchaguzi huu utaendeshwa kwa njia huru na wa haki. Baada ya uchaguzi huu kukamilika, wachambuzi wanashikilia kuwa, tume ya kusimamia uchaguzi italazimika kurekebisha vile ambavyo imekuwa ikiwasiliana na umma, kwani yalekea kuwa huo umekuwa upungufu wake mkubwa.
Mwandishi: Shisia Wassilwa/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef