1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yakabiliwa na upungufu wa sarafu ya dola

22 Machi 2023

Kenya inakabiliana na uhaba wa akiba ya fedha za kigeni. Wakati watumiaji wanahisi makali ya uhaba huu, matatizo makubwa zaidi ya kimuundo yanaendelea kuikumba nchi hiyo.

Libanon | Geldwechsel
Picha: Joseph Eid/AFP/Getty Images

Kenya ambayo ndiyo nchi yenye uchumi imara zaidi Afrika Mashariki, inakabiliwa na uhaba wa sarafu ya dola. Waagizaji wengi wa mafuta wanadai hawawezi kuagiza bidhaa hizo kwa sababu ya upungufu wa sarafu za kigeni.

Hali hii imepeleka uhaba katika maeneo muhimu kote nchini humo, hasa mji mkuu Nairobi, ambako dereva  Ibrahim Ngaumbua anasubiri katika foleni ndefu kujaza mafuta.

"Hiki ni kituo cha tatu cha mafuta nilichokitembelea, natafuta mafuta lakini inaonekana, hapa tuko Shell na wanasema ni V-power tu inayopatikana hapa, hivyo nimeamua tu kutumia V-power na sijui wapi naweza kupata petroli ya kawaida."

Kipi chanzo cha kupungua kwa hifadhi ya sarafu za kigeni?

Picha: Khaled Elfiqi/epa/dpa/picture alliance

Kupungua kwa hifadhi ya fedha za kigeni nchini Kenya kunalaumiwa kusababisha mzozo wa sasa unaowakabili watumaiji wa Kenya. Wa kwanza kuhisi maumivu hayo ni wafanyabiashara na waedenshaji magari wanaojaribu kujaza mafuta, huku baadhi ya vituo vya mafuta vikiishiwa petroli na dizeli, hasa mjini Nairobi.

Kwa sababu waagizaji wa mafuta wa Kenya wanatumia sarafu ya dola kununua mafuta, uhaba huo wa fedha za kigeni umekuwa na athari ya moja kwa moja kwenye ugavi wa mafuta nchini humo, na zaidi ya hapo, mfumo mzima wa ugavi nchini humo.

Lakini pia umeathiri bidhaa muhimu zinazotoka nje kama vile dawa na chakula. Bila pesa taslimu za kutosha, wafanyabiashara wakubwa na wadogo wanadai hawawezi kuagiza bidhaa.

Ester Mboni ni mfanyabiashara mdogo, "Kama waagizaji wadogo, tunaathiriwa na uhaba wa dola, vitu vyetu vingi hivi sasa vimekuwa ghali,na tunahitaji jambo lifanyike."

Wakati kukiwa na dola chache kwenye hifadhi, kiwango cha ubadilishaji kununua dola kwa shilingi ya Kenya kimepanda, katika baadhi ya kesi kwa zaidi ya asilimia 10.

Shilingi ya Kenya yashuka thamani

Hifadhi inayopungua ya fedha za kigeni nchini humo, ambayo imefikia rekodi ya miaka minane, imeiwekea pia mbinyo sarafu ya nchi hiyo dhidi ya sarafu nyingine kubwa kubwa.

Serikali inasema hakuna sababu ya kuhamaki, na kwamba kuna hifadhi ya kutosha ya pesa taslimu. Lakini Benki Kuu ya kenya imeziagiza benki za kibiashara kuanzisha mgao wa dola ili kulinda hifadhi.

Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Chanzo cha uhaba wa dola kimechangiwa na sababu mbalimbali - ikiwa ni pamoja na kushuka kwa mauzo ya nje, bili kubwa kutoka nje na kupungua kwa uhamishaji wa fedha - na kusababisha baadhi ya makampuni kutafuta fedha za kigeni katika nchi jirani ya Tanzania.

Wachambuzi wa masuala ya fedha, kama Wohoro Ndoho, wanaonya hali inaweza kuwa mbaya zaidi bila hatua madhubuti. Moja ya matatizo, kulingana na Ndoho, ni kwamba nchi za Afŕika zenye miradi mikubwa ya upanuzi wa miundombinu zimeingia madeni makubwa katika mazingira ambapo uwiano wa biashaŕa umeshuka kwa kiasi kikubwa, aliiambia DW.

Na kwa sababu dola ya Marekani ni sarafu taslimu inayopendelewa katika biashara ya kimataifa, mahitaji nchini Kenya ya dola kununua bidhaa zinazoagizwa kutoka nje yamesalia kuwa juu.

Zaidi ya hayo, kushuka kwa thamani ya shilingi ya Kenya kunaongeza gharama za uagizaji bidhaa na gharama za maisha, hivyo kuathiri faida ya biashara na ukuaji wa uchumi. Inaweza pia kuzuia uwezo wa serikali kutimiza majukumu yake ya deni la nje.

Wakati huo huo, hatua ya Benki Kuu ya Kenya kupunguza viwango vya riba inaweza kutoa unafuu wa muda mfupi.