1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroKenya

Kenya yailalamikia Urusi kuwapiganisha vita raia wake

10 Februari 2026

Serikali ya Kenya imewakemea mawakala wanaodanganya vijana kwa ahadi za kazi Urusi kisha kuwapeleka kupigana Ukraine. Wakenya wameuawa na kujeruhiwa, huku Nairobi ikipanga mazungumzo na Moscow kusitisha hali hiyo.

Kenya | Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi anapanga kwenda Urusi kuzungumzia utumiaji wa Wakenya kwenye vita dhidi ya UkrainePicha: Sebastian Gollnow/dpa/picture alliance

Kenya imelaani kama "jambo lisilokubalika" vitendo vya mawakala wa ajira wanaowashawishi Wakenya kwenda Urusi kwa ahadi za kazi zenye malipo mazuri, kisha kuwapeleka katika mstari wa mbele nchini Ukraine kama "chakula cha mizinga.”

Katika wiki za hivi karibuni, ripoti zinazoongezeka zinaonyesha kuwa Wakenya waliodanganywa kusafiri kwa kazi zenye mishahara mikubwa nchini Urusi wanakufa vitani, huku wengine wakipata majeraha mabaya.

Uchunguzi wa shirika la habari la Ufaransa, AFP, uliochapishwa wiki hii ulifichua mtandao wa udanganyifu uliowanasa wanaume wanne wasio na historia ya kijeshi — waliolazimishwa kusaini mikataba na jeshi la Urusi na kutumwa haraka mstari wa mbele Ukraine.

"Haikubaliki kwao kuwa washiriki katika mzozo huu,” Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Korir Sing'Oei aliiambia AFP.

Wanne hao, watatu wao wakirejea wakiwa wamejeruhiwa, walipewa mikataba iliyoandikwa kwa Kirusi. Mmoja alitarajia kufanya kazi kama muuzaji, wawili kama walinzi na wa nne kama mwanamichezo wa kiwango cha juu.

"Watu hawa wanatumika kama nyama ya mizinga katika mstari wa vita,” Sing'Oei alisema. "Hakuna Mkenya ambaye angeingia kwa hiari katika ushiriki wa aina hiyo.”

Vijana wengi wa Kenya waliahidiwa kwenda kufanya kazi zenye mshahara mnono nchini Urusi na kuishia kupelekwa uwanja wa mapambano dhidi ya Ukraine.Picha: Michal Dyjuk/AP/picture alliance

Waziri Mudavadi kwenda Moscow kuyajadili

Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi alitangaza kwamba atasafiri kwenda Moscow kwa mazungumzo yanayolenga "kumaliza kabisa suala hili na kubaini suluhu endelevu.”

"Tumeona upotevu wa maisha, na ninapanga kufanya ziara Moscow ili kusisitiza kuwa hili ni jambo linalopaswa kusitishwa,” Mudavadi alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Alisema pia atafuatilia kuachiliwa kwa Wakenya waliokamatwa kama wafungwa wa kivita nchini Ukraine na "kuthibitisha” hali ya waliolazwa hospitalini.

Mudavadi alisema zaidi ya Wakenya 30 wamehamishwa kutoka Urusi katika miezi miwili iliyopita na mashirika yasiyo waaminifu ya ajira nchini Kenya yamefungwa.

Mvuto wa mikataba ya kazi ya uongo

Shirika la Utangazaji wa Umma la Ujerumani, ZDF, liliripoti kuwa Moscow inatumia mbinu zisizo za haki kujaza safu zake za wanajeshi kwa vita vya Ukraine. Wanaume kutoka nchi kama India na Kenya wanasema walivutwa kwa ahadi za kazi zisizo za kweli. Kremlin inadai walijiunga kwa hiari.

Mwandishi wa ZDF Afrika Susan von Lojewski alitembelea kijiji cha Charles Waithaka mwenye umri wa miaka 31 katikati mwa Kenya. Alivutwa kwenda Urusi kwa ahadi ya kufanya kazi kama fundi kwa jeshi la Urusi. Muda mfupi baada ya kuwasili, aliwasilishiwa mkataba mpya — kwa Kirusi.

Mwanafunzi kutoka Togo asota gerezani Ukraine

02:10

This browser does not support the video element.

Baada ya mafunzo mafupi ya kijeshi, alitumwa kama mwanajeshi kwenye mpaka wa Urusi na Ukraine, ambako aliuawa na bomu la ardhini.

Waziri Mudavadi aliiambia ZDF kuwa wameiomba serikali ya Urusi kuhakikisha Wakenya wanaondolewa kwenye orodha ya wanaoweza kuajiriwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW