1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yamuaga kiserikali rais wa zamani Kibaki

29 Aprili 2022

Mwili wa marehemu rais wa zamani wa Kenya, Mwai Kibaki, unasubiria maziko siku ya Jumapili kijijini kwao Othaya, Kaunti ya Nyeri. Ibada maalum ya kumuaga jijini Nairobi ilifanyika uwanja wa michezo wa kitaifa wa Nyayo

Kenia Beisetzung Ex-Präsident Mwai Kibaki
Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Viongozi wa ngazi ya juu wa ndani na nje ya serikali kuu ya Kenya walifika uwanjani kuifariji familia. Nchi jirani ya Tanzania imetangaza siku mbili za maombolezi ya taifa. Rais huyo wa tatu wa Kenya alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 90. Maelfu ya Wakenya walipambana na kibaridi cha asubuhi kufika kwenye uwanja wa michezo wa Nyayo kumuaga rais wao wa tatu Mwai Kibaki.

Soma pia:Kenyatta: Awaongoza wakenya kumuaga aliekuwa Rais wa taifa hilo Kibaki Bungeni

Msafara wake uliondoka kwenye nyumba ya kuhifadhia maiti mwendo wa saa mbili asubuhi na kupokelewa na kiongozi wa taifa aliyekuwako na mkewe, Mama Margaret, kwenye ikulu ya Nairobi. Wana wanne wa marehemu Rais Kibaki waliovalia sare nyeusi nao pia waliusindikiza msafara huo uliolibeba jeneza lililofinikwa na bendera ya taifa.

Wakuu mbalimbali wa nchi walihudhuria ibada Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Ibada maalum ya mchanganyiko ilisimamiwa na askofu mkuu wa Kanisa Katoliki Philip Anyolo aliyeshirikiana na mwenzake wa Kanisa la Mombasa Paul Kivuva kuongoza misa.

Itakumbukwa kuwa marehemu rais wa tatu wa Kenya alikuwa mkatoliki na hakuwahi kukosa kuhudhuria misa kila alipojikuta kwenye Kaunti ya Nyeri alikotokea wakati wa siku ya ibada. Viongozi wa kanisa katoliki waliusisitizia umuhimu wa kuvumiliana kama alivyofanya marehemu rais Kibaki.

Soma pia: Kipi atakachokumbukwa nacho Mwai Kibaki?

Mwanawe David Kagai alimsifu marehemu Rais Kibaki kwa kuwa si tu baba na mzazi mzuri bali pia mwandani wake. Kauli hizo zinaungwa mkono na viongozi waliofika kutoa heshima zao za mwisho. Viongozi wa jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na rais wa Afrika Kusini na mwenzake wa Ethiopia walikuwako ibadani. Naibu wa Rais William Ruto alimsifu marehemu Kibaki kama muasisi wa mikakati ya maendeleo ya serikali ya Jubilee.

Kiongozi wa taifa rais Uhuru Kenyatta alimsifu mtangulizi wake kwa kuwa kiongozi mzuri aliyevumilia mengi bila papara. Maiti ya marehemu Rais Kibaki itasafirishwa kwa barabara hadi Othaya, Nyeri siku ya Jumamosi atakakozikwa kwao kijijini. TM, DW Nairobi.

Thelma Mwadzaya, DW Nairobi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW