1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaomboleza kifo cha Raila Odinga

Shisia Wasilwa
15 Oktoba 2025

Taifa la Kenya linaomboleza kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Amolo Odinga, mwamba wa siasa na nembo ya demokrasia, aliyefariki dunia hii leo Jumatano (15.10.2025) Kerala, India, akiwa na umri wa miaka 80.

Kenya yaomboleza kifo cha Raila Odinga
Kenya yaomboleza kifo cha Raila Odinga Kiongozi wa chama cha upinzani ODM Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Kwa mujibu wa taarifa za uongozi wa hospitali hiyo ya nchini India, Odinga alipoteza fahamu wakati wa matembezi ya asubuhi katika eneo la kituo cha tiba asilia "Ayurveda" kilichopo Koothattukulam, katika wilaya ya Ernakulam, katikati ya mji wa Kerala alipokuwa anatibiwa.

Mwili wake Raila umehifadhiwa katika hospitali binafsi mjini Kochi chini ya ulinzi wa polisi, huku maandalizi ya kidiplomasia na kifamilia ya kusafirisha mwili wake kurejeshwa Kenya yakiendelea. Licha ya juhudi za haraka za madaktari, alitangazwa kufariki dunia saa tisa na dakika 52 alfajiri kwa saa za India kutokana na mshutuko wa moyo.

Tangazo la kifo cha Odinga limeitumbukiza Kenya katika majonzi makubwa, huku salamu za rambirambi zikimiminika kutoka pande zote za kisiasa na jumuiya ya kimataifa. Akiwa anajulikana kwa jina la upendo Baba, lenye maana ya baba wa taifa, Raila Odinga alionekana kama moyo wa mapambano ya Kenya kwa ajili ya haki, vyama vingi na mageuzi ya kisiasa.

William Ruto: Taifa limempoteza mzalendo na mwanamageuzi wa kweli

Rais William Ruto aliongoza taifa kuomboleza, akimtaja Odinga kuwa "mzalendo wa taifa ambaye ujasiri na kujitolea kwake viliunda njia ya Kenya kuelekea demokrasia na umoja.” Viongozi kutoka barani Afrika akiwemo Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Nana Akufo-Addo wa Ghana na Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, walimsifu Odinga kama "mwanafalsafa wa Uafrika aliyechochea kizazi cha viongozi wenye maono.”

Rais wa Kenya William Ruto aliongoza taifa kuomboleza kifo cha Raila Odinga aliyekuwa Waziri Mkuu wa taifa hilo la Afrika Mashariki Picha: JOSPIN MWISHA/epd/IMAGO

Habari za kifo chake ziliposambaa, hisia kali za huzuni ziliripotiwa jijini Nairobi, Kisumu na Bondo, ambako maelfu walifurika mitaani wakiwa na bendera, mishumaa na nyimbo za ukombozi kumkumbuka kiongozi huyo.

Mitandao ya kijamii imefurika na ujumbe wa rambirambi kutoka ndani na nje ya nchi, watu wakikumbuka hotuba zake zenye moto, ucheshi wake, na uzalendo usiokuwa na mipaka. Familia ya Odinga imeomba faragha wanapojaribu kukabiliana na pigo hili, huku serikali ikianza maandalizi ya mazishi ya kitaifa, kumuenzi mmoja wa viongozi mashuhuri zaidi wa Kenya.

Raila mpambanaji na mwanamapinduzi

Katika jangwa la siasa za Kenya, jina Raila Amolo Odinga limekuwa kama ngurumo ya radi kabla ya mvua, sauti iliyotikisa milima ya mamlaka na mabonde ya ukosefu wa haki.

Raila Odinga aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya aaga dunia akiwa nchini India Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Raila hakuwa mwanasiasa wa kawaida, alikuwa mchecheto wa mapambano, kiongozi aliyezaliwa kwa upepo wa vuguvugu na mwanamapinduzi aliyeandika jina lake kwa wino wa uvumilivu. Philip Okiyai ni mtaalamu wa masuala ya uongozi.

"Mimi kama Mkenya nitamkumbuka raila kama shujaa aliyepigania demokrasia na mabadiliko ya Katiba. Leo ni siku ya huzuni naomboleza kifo chake.”

Raila Odinga alizaliwa Januari 7, 1945, Raila Odinga. Alikuwa mwana wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Kenya, Jaramogi Oginga Odinga. Alirithi si tu jina la familia lenye uzito wa kisiasa, bali pia moyo usiyotetereka wa kupigania haki. Katika miaka ya 1980, Raila alikabiliwa na vipindi virefu vya kizuizini chini ya utawala wa Rais Moi, kutokana na harakati zake za kudai demokrasia.