1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaondoa marufuku ya kutembea usiku

Shisia wasilwa20 Oktoba 2021

Rais Uhuru Kenyatta ameondoa marufuku ya kutembea usiku ambayo imekuwepo tangu mwaka 2020. Kenyatta ametangaza hilo alipoiongoza nchi yake kuadhimisha siku ya Mashujaa.

Kenias Präsident Uhuru Kenyatta
Picha: picture-alliance/B.Inganga

Rais Kenyatta ameiongoza Kenya kuadhimisha siku ya mashujaa huku akitangaza kwamba ameondoa marufuku ya kutembea usiku ambayo imekuwepo tangu mwaka 2020. Sherehe hiyo iliyofanyikia katika jimbo la Kirinyaga, ilihudhuriwa na rais wa Malawi Lazurus Chakwera na viongozi wa upinzani nchini humo.

Wakenya wa matabaka mbali mbali walivumilia mvua na kibaridi kikali katika uwanja wa Wang'uru, ulioko katika jimbo la Kirinyaga, na kuhudhuria sherehe ya 58 ya mashujaa awali ikijulikana kuwa siku ya Kenyatta. Ni sherehe ambayo huwakumbuka waasisi wa taifa hilo waliopigana kumtimua beberu pamoja na wakenya waliofaulu katika Nyanja mbali mbali.

Akilihutubia taifa, Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa, serikali yake imeweka mikakati kadhaa ya kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Tamko lake likijiri wakati ambapo uchumi wa kenya ukiyumba kutokana na marufuku ya kutembea usiku ambayo imekuwa ikizingatiwa kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri. Kufungwa uchumi wa taifa ambao ulikuwa umefungwa kwa kipindi kirefu kumekuwa na athari hasi kwa Wakenya wengi.

Wakenya wengi wamelipokea tangazo la Rais Kenyatta la kuondoa marufuku kwa furahaPicha: Dai Kurokawa/epa/dpa/picture alliance

"Ninaamuru kafyuu ya taifa ya kutotoka nje ambayo imekuwepo tangu mwaka 2020 kuanzia usiku hadi alfajiri iondolewe mara moja," amesema Kenyatta.

Katika kipindi cha majuma matatu yaliyopita, maambukizi ya virusi vya corona yamepungua kwa asilimia tano, huku idadi ya watu waliopata chanjo ikiongezeka na kufikia watu milioni 1.2.

Idadi ya waumini kwenye maabadi pia imeongezwa kutoka thuluthi moja hadi thuluthi mbili. Kuanzia tarehe mosi Novemba mwaka huu, serikali ya Kenya itatoa fedha za kuchochea sekta za Kilimo, Elimu na maeneo yaliyokumbwa na ukame.

Marufuku ya kutembea usiku ilikuwa imeathiri shughuli ambazo huendeshwa usiku huku biashara nyingi zikifungwa mwendo wa saa mbili. Zaidi ya mabaa 15000 na vituo vya burudani vilifungwa wakati janga la covid 19, lilipotangazwa huku watu 90000 wakipoteza ajira.

Hata hivyo Wakenya wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo. Rais Lazarus Chikwera wa Malawi ambaye yuko Kenya kwa ziara ya siku tatu alikuwa mgeni mwalikwa huku akiandamana na mkewe Monica Chakwera.

Wafanyabiashara mbalimbali, wasanii na wahudumu katika kumbi za burudani ni miongoni mwa wale ambao wamelalamikia marufuku ya kutoka nje nchini Kenya ambayo imekuwepo tangu Machi 2020.Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

"Malawi na Kenya ni ndugu wa miaka mingi sana, tangia wakati wa baba zetu, mzee Jommo Kenyatta wa Kenya na mzee Kamuzu Banda wa Malawi. Kutembelea Kenya leo ni uthibitisho wa udugu na umoja wetu,” amesema Chakwera.

Kama ishara ya mshikamano na utangamano wa taifa, viongozi wa upinzani walihudhuria, wakiongozwa na Raila Odinga wa ODM, Musalia Mudavadi Kiongozi wa Amani National Congress, Gideon Moi Kiongozi wa chama cha KANU na Moses Wetangala kiongozi wa Ford Kenya. Makamu wa Rais William Ruto ambaye ameonekana kutofautiana na Rais Kenyatta akiendelea kujipigia debe.

"Nakuhakikishia mheshimiwa Rais, kwamba nitaendeleza urithi wako na ajenda nne kuu za kubadilisha taifa kupitia mmfumo wa kuwa kuwajali wanyonge,” amesema Ruto.

Rais Kenyatta anatarajiwa kukita kambi katika eneo hilo la Mlima Kenya, kwa lengo la kutoa mwelekeo wa siasa za mwaka ujao, kwani yaelekea halijapata msemaji, pindi atakapoachia mikoba ya uongozi.