Kenya yaondoa masharti ya mwisho ya Covid-19
11 Machi 2022Agizo la kuvaa barakoa kila wakati lilitangazwa mwanzoni mwa Aprili miaka miwili iliyopita. Akizungumza na waandishi wa habari hapa jijini Nairobi, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesisitiza kuwa ipo haja ya kuendelea kuwa makini na kufuata maagizo yaliyopo ya kuepuka kutangamana na kusambaza COVID 19.
Waziri wa afya wa Kenya ameusisitizia umma umuhimu wa chanjo kwenye mapambano dhidi ya COVID 19. Kadhalika hatua za kuwatenga walioambukizwa homa hiyo kali nazo pia zimeondolewa na sio lazma kuwekwa karantini.
Walioambukizwa COVID 19 ila hawana ishara zozote nao pia hawalazimiki kutengwa kwenye maeneo maalum bali watatazamwa kwa siku 5 na kurejea kwenye shughuli zao za kawaida pasi na vipimo vya kufuatilia. Je wakenya wanasemaje kuhusu tangazo hilo la kutoshurutishwa kuvaa barakoa? Baadhi nliozungumza nao walikuwa na haya ya kusema.
Duru zinaeleza kuwa idadi ya maambukizi mapya imepungua na kufikia 0.2% hali ambayo inaufuta ulazima wa kupima viwango vya joto la mwili kabla kuingia kwenye maeneo ya umma. Hata hivyo ipo mitazamo tofauti ukizingatia kuwa serikali ya Kenya imetangaza siku chache zilizopita uzinduzi wa kiwanda cha kutengeza chanjo na vidonge vya kupambana na COVID 19.
Marufuku ya watu kutembea nje wakati wa usiku iliondolewa mwaka uliopita wakati wa maadhimisho ya siku ya Mashujaa. Kufikia sasa takwimu za Wizara ya afya zinaashiria kuwa maafa ya COVID 19 yamefikia 5,644 ila idadi ya watu wazima waliochanjwa bado iko 28.5% ya wakenya wote ambayo inasadikika kuwa ndogo. Ken Bundi Miriti ni mratibu wa afya na anaelezea kuhusu chanjo ya COVID 19. Azma ya serikali ya Kenya ni kuwachanja watu wasiopungua milioni 27 ifikapo mwezi wa Juni mwaka huu.