1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaondoa vikwazo dhidi ya bidhaa za Tanzania

24 Julai 2017

Kenya imeondoa marufuku iliyoweka dhidi ya unga wa ngano na gesi ya kupikia kutoka Tanzania. Tanzania nayo imeiruhusu Kenya kuiuzia maziwa na sigara.

Tansania - Dr. Augustine Mahiga
Picha: DW

Kenya imeondoa marufuku ya unga wa ngano na gesi ya kupikia kutoka Tanzania na wakati huo huo Tanzania kuruhusu Kenya kuliuzia taifa hilo maziwa na sigara. Hayo yaliafikiwa jijini Nairobi kufuatia mazungumzo kati ya rais Uhuru Kenyatta na John Pombe Magufuli. Ujumbe kuhusu mazungumzo ya viongozi hao ulitangazwa na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili waliozungumza na waandishi habari.

Hatua ya Kenya na Tanzania ya kuondoa marufuku ya kuagiza na kuuza bidhaa zake, inalenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia ambao wachambuzi wanasema  unasuasua. Kwenye hatua hiyo, Kenya sasa imeruhusiwa kuuza maziwa na sukari kwa taifa la Tanzania huku Tanzania ikiruhusiwa kuiuzia Kenya Unga wa ngano na gesi ya kupikia. Waziri wa masuala ya nje wa Tanzania Augustine Mahiga aliyemuwakilisha Rais John Pombe Magufuli amethibitisha hayo.

Hata hivyo Wakenya watahitaji kuomba kibali cha Viza ili kuruhusiwa kuingia nchini Tanzania, suala ambalo Mahiga alisema taifa lake lingali linalijadili, hatua ambayo inatia doa uhusiano wa mataifa hayo.

Maafisa wa bodi ya shirika la mafuta Tanzania TPDC wakielezewa kuhusu namna gesi husafirishwa kwa mabomba kufikia watumiziPicha: DW/Z. Musa

Mataifa hayo mawili yataendelea kutoa ulinzi wa pamoja kwenye mipaka huku hati ya usafiri ya jumuiya ya Afrika Mashariki ikirahisisha usafiri kati ya mataifa ya jumuiya. Kenya na Tanzania zilikubaliana kuweka kamati ya pamoja itakayoongozwa na mawaziri wa masuala ya kigeni itakayojumuisha mawaziri wa masuala ya Afrika mashariki, biashara, fedha, usalama, kilimo na utalii. Kwa upande wa Kenya, Amina Mohammed alimuwakilisha rais Uhuru Kenyatta.

Kenya ilipiga marufuku uagizaji wa gesi kutoka Tanzania mwezi Aprili, huku wizara ya nishati nchini Kenya ikisema hatua hiyo ililenga kukabiliana na ongezeko la viwanda bandia. Kampuni za gesi za Tanzania huiuzia Kenya tani elfu 40 ya gesi kila mwaka. Gesi ya Tanzania ni bei nafuu kwa sababu gharama za upakuaji wake katika bandari za Tanga na Dar Es Salaam ni nafuu ikilinganishwa na  bandari ya Mombasa. Mauzo ya Kenya kwa mataifa ya kanda hii yamepungua katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kwa mujibu wa takwimu mpya. Aidha bidhaa ambazo Tanzania inaagiza kutoka Kenya zilipungua kutoka dola milioni 78 hadi dola milioni 67.5 katika kipindi hicho.

Mwandishi: Shisia Wasilwa

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW