1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
BiasharaKenya

Maembe ya Makueni yafungua ukurasa mpya Uingereza

7 Machi 2026

Baada ya marufuku ya miaka kumi, Kenya imerejea kwenye soko la kimataifa la maembe. Wakulima wa kaunti ya Makueni wanashuhudia afueni huku tani 4,900 zikisafirishwa kwenda nchini Uingereza mwanzoni mwa mwaka huu.

Wakulima kutoka Makueni, Kenya wakibeba maembe
Wakulima kutoka Makueni, Kenya wakibeba maembePicha: Thelma Mwadzaya/DW

Kenya imerejea kwenye soko la kimataifa la maembebaada ya kuweka marufuku ya kujilinda kwa muda wa muongo mmoja. Wakulima wa maembe katika kaunti ya Makueni wamepata afueni kufuatia kupatikana kwa soko jipya nchini Uingereza. Shehena ya kwanza iliondoka mwanzoni mwa mwaka huu, ikifungua ukurasa mpya kwa wakulima.

Ni msimu wa maembe katika kaunti ya Makueni na mashamba mengi yamesheheni matunda. Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya tani 4,900 za maembe zilisafirishwa kwenda Uingereza mapema mwaka huu. Redempta Kitili wa shirika la Maatha anasema mafunzo kutoka TradeMark Africa yaliwasaidia kuboresha ubora wa maembe na kuyafanya yakubalike katika soko la nje.

Mti wa maembe aina ya Apple huko Makueni, KenyaPicha: Thelma Mwadzaya/DW

Safari ya mabonde na milima

Hata hivyo, safari haikuwa rahisi. Mdudu waharibifu aliyekuwa akishambulia maembe ulisababisha hasara kubwa na kuchangia kupotea kwa soko la kimataifa kwa takribani miaka kumi. Josephine Mutisya, mkulima mkongwe, anasema mafunzo ya matumizi sahihi ya dawa na mbolea yameleta mabadiliko, lakini soko bado ni changamoto.

Serikali iliweka marufuku ya usafirishaji ili kulinda hadhi ya maembe ya Kenya. Kwa ushirikiano na wadau, wakulima walipewa mafunzo ya kufuata viwango vya kimataifa. Dr. Andrew Edewa wa TradeMark Africa anasema hatua kama kuogesha maembe kwenye maji ya moto na kuzingatia usafi zimewezesha mazao kukidhi vigezo vya Ulaya.

Serikali ya kaunti ya Makueni pia imewekeza katika mafunzo, kiwanda cha juisi, na kupunguza ada za biashara. Waziri wa kilimo Elizabeth Muli anasema zaidi ya wakulima 10,000 wamepata mafunzo ili kuongeza ubora na thamani ya zao hilo.

Soko la nje na matumaini mapya

Uingereza sasa ni miongoni mwa masoko muhimu ya maembe ya Kenya barani Ulaya. Anne Nalo wa ubalozi wa Uingereza anaeleza kuwa ushirikiano huo umejenga imani mpya ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Wakulima wakikagua maembe Makueni, KenyaPicha: Thelma Mwadzaya/DW

Aina zinazopendwa zaidi ni Apple na Kent. Wafanyabiashara kama Ganel Gaute wanaona fursa mpya, wakisisitiza umuhimu wa wakulima kuelewa taratibu za soko la kimataifa.

Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa, tani zaidi ya 650,000 za maembe huvunwa kila mwaka nchini Kenya. Hata hivyo, changamoto kama bei duni, uhaba wa wanunuzi na madalali bado zinawakwamisha wakulima wadogo.

Wakulima kama Steven Mutinda na Julius John wanasema mafunzo ya kilimo endelevu yamewasaidia kulinda mazingira na kuboresha uzalishaji. Licha ya changamoto, wana matumaini kuwa soko la kimataifa litaendelea kupanuka.

TradeMark Africa inaamini kuwa mafanikio haya ni mwanzo wa fursa zaidi za kusafirisha maembe na mazao mengine barani Ulaya kupitia mipango ya kibiashara kama BEEP.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW