1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaridhia kufunguliwa kwa hoteli na mikahawa

Thelma Mwadzaya27 Aprili 2020

Wafanyabiashara wa hoteli na mikahawa wanafungua ukurasa mpya baada ya serikali kutoa ridhaa ifunguliwe kuanzia alfajiri hadi alasiri.

Kenia Mutahi Kagwe
Waziri wa Afya nchini Kenya Mutahi KagwePicha: picture-alliance/ZUMAPRESS/D. Sigwe

 

Kenya pia imepata fursa kuwa miongoni mwa mataifa yaliyoruhusiwa kufanya majaribio ya dawa nne kwa ajili ya wagonjwa wa COVID-19 waliolazwa. Idadi ya maambukizi imefikia 363.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye afisi yake, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amethibitisha kuwa watu wengine wanane wameambukizwa kufikia leo.Visa hivyo vimeripotiwa kutokea Nairobi na Mombasa. Hata hivyo,114 walioambukizwa wamepona.

Wagonjwa hao wanane wapya walioambukizwa Corona wanaripotiwa kuwa hawakusafiri kokote nje ya nchi. Yote hayo yakiendelea, Kenya imepata nafasi ya kuwa kwenye orodha ya mataifa yatakayoweza kufanya majaribio ya hospitali ya dawa nne kwa ajili ya COVID 19.
Hata hivyo wagonjwa hao sharti wawe na umri usiopungua miaka 18, wamelazwa hospitali kwa sababu ya COVID 19 na hawajapokea dawa nyengine zozote kupambana na hali hiyo. Dawa hizo nne ni Remdesevir, Lopinavir, Ritonavir na Chloroqiune.

Matokeo ya majaribio hayo ya hospitali yanatazamiwa kutangazwa mwezi Machi mwaka ujao.

Wabunge wasusia kupitisha mswada utakaowalazimu Wakenya kulipa faini kwa kutovaa barakoa

Kiongozi wa wengi katika bunge la Kenya Aden DualePicha: Reuters/T. Mukoya

Kwa upande mwengine, wabunge wamesusia kupitisha mswada utakaowalazimu Wakenya kulipa faini ya shilingi alfu 20 kwa kutovaa barakoa mtaani.

Kadhalika wanaopatikana wakikiuka amri ya kutotoka nje usiku wanatozwa faini ya shilingi alfu moja na kupelekwa kwenye karantini kwa lazima jambo ambalo pia wabunge wamelikataa.

Badala yake wamemtaka Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na mwenzake wa usalama wa taifa, Dk. Fred Matiangi, kufika mbele ya Kamati ya Bunge ya Sheria ya muda kujieleza.

Hatimaye shule zitaendelea kufungwa kwa mwezi huu wakati ambapo muhula wa pili unaanza. Shule zilifungwa pindi tangazo la kisa cha kwanza cha maambukizo kutangazwa mwanzoni mwa Machi.

Amri ya kutotoka nje kuanzia magharibi hadi alfajiri inaingia awamu yake ya pili kwa siku 21 zijazo.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW