1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yathibitisha Tanzania imemuachia Boniface Mwangi

22 Mei 2025

Baada ya siku kadhaa za kuzuiliwa bila mawasiliano, mwanaharakati maarufu wa Kenya Boniface Mwangi aliachiwa na mamlaka za Tanzania huku hofu kuhusu ukandamizaji wa haki za kiraia ikitanda kanda nzima.

Kenya | Boniface Mwangi
Mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi (katikati) akiongoza maandamano nchini mwake, Februari 13, 2024.Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Mamlaka za Tanzania zimemuachia huru mwanaharakati mashuhuri wa Kenya, Boniface Mwangi, ambaye alikuwa amekamatwa na kushikiliwa kwa siku kadhaa bila kuwasiliana na mtu yeyote.

Mwangi alikuwa ameenda jijini Dar es Salaam kuonesha mshikamano kwa kiongozi wa upinzani wa Tanzania, Tundu Lissu, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhaini.

Kwa mujibu wa shirika la Amnesty International, Mwangi na mwandishi wa habari kutoka Uganda, Agatha Atuhaire, walikamatwa Jumatatu na kushikiliwa na maafisa wa kijeshi, bila kufikishwa mahakamani wala kujulisha familia zao walipopelekwa.

Soma pia: Wanaharakati wazuiliwa Tanzania: Sakata la kesi ya Tundu Lissu lazua mjadala mpana

Alhamisi wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, alithibitisha kuwa Mwangi aliachiwa. Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi kuhusu mazingira ya kuachiliwa kwake, akisema tu kuwa "tumejihusisha kidiplomasia, na ndivyo inavyofanyika."

Gazeti la Daily Nation linaripoti kuwa Mwangi alirudishwa Kenya kwa barabara na kutelekezwa katika mji wa Ukunda, karibu na mpaka wa Tanzania. Alikimbizwa hospitalini kwa uchunguzi, ambapo mkewe, Njeri Mwangi, alisema mumewe amejeruhiwa na miguu yake imevimba.

Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Musalia Mudavadi amafahamisha kuwa Mwangi ameachiliwa na mamlaka za TanzaniaPicha: Sebastian Gollnow/dpa/picture alliance

Wito wa kitaifa na kimataifa watikisa serikali

Kukamatwa kwa Mwangi kulizua taharuki kubwa nchini Kenya. Takribani mashirika 20 ya haki za binadamu yalitoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka kumtetea na kumrejesha nyumbani bila masharti.

Shirika la Amnesty lilieleza kuwa mawakili wa Mwangi na Atuhaire walijulishwa awali kuwa walikuwa karibu kuondolewa nchini kwa ndege, lakini tangu hapo mamlaka za Tanzania zilinyamaza kimya, hali iliyoibua hofu kuwa walitekwa nyara.

Kwa upande wa Uganda, Balozi wake nchini Tanzania, Fred Mwesigye, alisema kuwa bado walikuwa wakisubiri majibu kutoka kwa serikali ya Tanzania kuhusu hali ya Agatha Atuhaire. Haikubainika mara moja iwapo na yeye aliachiwa au la.

Soma pia: Kenya yataka waliokamatwa Tanzania kuachiwa huru

Katika mahojiano ya awali, mke wa Mwangi alikanusha taarifa kuwa mumewe alikuwa anasafirishwa kwa ndege, akisema kuwa polisi walikuwa wakitoa taarifa zinazopingana huku wanamshikilia kwa siri.

Siyo jambo la Nadra kwa Mwangi kukabiliana na mamlaka za usalama. Katika picha ya mwaka 2013, mwanaharakati huyo anaoneka akishikiliwa na polisi wakati wa maandamano ya kupinga mishahara mikubwa kwa wabunge nchini Kenya.Picha: Carl de Souza/AFP/Getty Images

Serikali ya Tanzania yasimamia msimamo mkali

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alisema mapema wiki hii kuwa "watu wasio na adabu kutoka nchi nyingine" hawataruhusiwa kuvuka mipaka ya Tanzania na kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo. Alizitaka taasisi za usalama kutowapa nafasi watu wa aina hiyo.

Wakati huo huo, chama cha upinzani cha Chadema, ambacho Tundu Lissu ni mwanachama wake, kimepigwa marufuku kushiriki uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba, baada ya kukataa kusaini kanuni za ushiriki kikishinikiza marekebisho ya mfumo wa uchaguzi.

Viongozi wengine wa upinzani kutoka nje ya nchi, akiwemo Martha Karua wa Kenya, walizuiwa kuingia nchini Tanzania kupitia uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na kurejeshwa walikotoka kabla ya kesi ya Lissu.

Wataalamu: Huu ni muendelezo wa kukandamiza Demokrasia

Mashirika ya haki za binadamu na wachambuzi wanasema tukio hili ni sehemu ya mwelekeo mpana wa kuzorota kwa demokrasia Afrika Mashariki. Hali kama hiyo inashuhudiwa pia Uganda, ambako kiongozi wa upinzani, Kizza Besigye, anakabiliwa na kesi ya uhaini baada ya kudaiwa kutekwa nyara nchini Kenya na kupelekwa Uganda.

Maraga afika mahakamani kusikiliza kesi ya Lissu

00:48

This browser does not support the video element.

Karua, ambaye pia ni wakili katika kesi ya Besigye, amesema hali inayoshuhudiwa Tanzania na Uganda inadhihirisha hatari inayoukumba uhuru wa kiraia na kisiasa katika ukanda huu.

Soma pia: Mamlaka Kenya zakanusha kuwateka wakosoaji wa serikali

Wito umeendelea kutolewa kwa jumuiya ya kimataifa na vyombo vya habari vya kimataifa kushinikiza serikali za Afrika Mashariki kuheshimu haki za binadamu, uhuru wa kujieleza, na uhuru wa kushiriki katika shughuli za kisiasa bila hofu ya kukamatwa au kushambuliwa.

Kwa sasa, ingawa Boniface Mwangi yuko huru, taswira kubwa ya ukandamizaji wa wanaharakati inaendelea kuibua maswali kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa ukanda huu unaoelekea katika uchaguzi muhimu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW