1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yashinda medali ya dhahabu katika Olimpiki

Sylvia Mwehozi
6 Agosti 2024

Mwanariadha wa Kenya Beatrice Chebet ameshinda mbio za mita 5,000 za Olimpiki upande wa wanawake na kutwaa medali ya dhahabu baada ya kumbwaga mwanariadha mwingine wa Kenya.

Faith Kipyegon (Goldmedaille in Budapest im 1.500m Lauf)
Picha: imago images

Mwanariadha wa Kenya Beatrice Chebet ameshinda mbio za mita 5,000 za Olimpiki upande wa wanawake na kutwaa medali ya dhahabu baada ya kumbwaga mwanariadha mwingine wa Kenya na bingwa wa dunia Faith Kipyegon ambaye alifutiwa ushindi wake kabla ya kurejeshewa.

Kipyegon ambaye ni mshindi wa medali ya dhahabu ya mita 1,500 mara mbili aliongoza raundi ya mwisho ya mbio hizo akiwa amesaliwa tu na mita chache kabla ya mstari wa mwisho lakini Chebet ambaye anashikilia rekodi ya dunia ya mita 10,000 alikuwa na nguvu zaidi na kumshinda.

Soma: Olimpiki: Kenya yaandamwa na kivuli cha kututumua misuli

Awali, Kipyegon aliyekuwa amemaliza nafasi ya pili alifutiwa ushindi wake kufuatia madai ya kumsukuma bingwa mwingine wa rekodi ya dunia kutoka Ethiopia Gudaf Tsegay wakati wa raundi mbili za mwisho. Baadae alirejeshewa ushindi wake na hivyo kurekodiwa kama mshindi wa pili wa mbio za mita 5,000 na kujinyakulia medali ya fedha. Maafisa wa timu ya Kenya waliwasilisha pingamizi dhidi ya kufutwa ushindi wa mwanariadha wao Kipyegon.

Bingwa wa Olimpiki Eliud Kipchoge wakati wa mbio za marathon za BerlinPicha: Christoph Soeder/AP

Kufuatia rufaa hiyo, mwanariadha wa Uholanzi Sifan Hassan aliyekuwa amepewa medali ya fedha alishushwa na kusogea katika nafasi yake ya tatu na kubeba medali ya shaba. Sifan mwenye umri wa miaka 31, alikuwa na matumaini ya kuwa mwanamke wa kwanza katika historia kushinda medali ya dhahabu ya mita 5,000, 10,000 na marathon katika michezo hii ya Olimpiki, akiiga mafanikio yaliyofikiwa na bingwa wa mbio za masafa marefu upande wa wanaume Emile Zatopek katika Michezo ya mwaka 1952 huko Helsinki.

Wanariadha wa Ethiopia safari hawakuwa na makali ambapo Ejgayehu Tayu alimaliza nafasi ya tano na Gudaf Tsegay nafasi ya nane. Ushindi wa Chebet unaifanya Kenya kuweka kibindoni medali ya kwanza ya dhahabu katika michezo hiyo ya Olimpiki ya Paris mwaka 2024. China bado inaongoza jedwali la medali ikifuatiwa na Marekani na nafasi ya tatu ni Australia.Kenya yashinda medali mbili za dhahabu London Marathon

Mwanariadha wa Uingereza Keely Hodgkinson alitawala fainali ya Olimpiki ya mita 800 na kushinda dhahabu mjini Paris na kuhitimisha ukame wa taji la kimataifa. Tsige Duguma wa Ethiopia alishinda medali ya fedha, huku bingwa wa dunia Mary Moraa kutoka Kenya akimaliza wa tatu kwenye Uwanja wa Stade de France.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW