1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yatangaza operesheni mpya ya usalama

Wakio Mbogho4 Februari 2022

Waziri wa usalama wa ndani wa Kenya Fred Matiangi ametangaza kuwa nchi hiyo itaanza oparesheni mpya ya usalama kuikabili hali ya mashambulizi ya mara kwa mara katika maeneo kadhaa.

Kenia | Drogenhandel | Fred Matiang'i
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Vikosi vya usalama kuanzia kesho vitaanza zoezi la siku 14 la kuwafurusha wavamizi na kurejesha hali ya utulivu kwenye maeneo ya Elgeyo Marakwet, Baringo na Pokot Magharibi ambayo yamekumbwa na uvamizi. Akizungumza baada ya mkutano na viongozi wa umma na wa kisiasa kutoka maeneo hayo, Waziri wa usalama wa ndani Fred Matiangi amesema jopo kazi maalum lililoundwa litafanya oparesheni ya anga na ya ardhini. Watatumia vyombo vya kisasa na kuajiri polisi wa akiba, ili kuweza kuimarisha usalama hasa kwenye shule ndiposa ziweze kufungua na wanafunzi waendelee na masomo.

Zaidi ya watu saba wamefariki katika muda wa mwezi mmoja pekee. Waziri Matiangi ambaye aliandamana na Inspekta mkuu wa polisi Hillary Mutyambai, amezungumzia umuhimu wa kuzihusisha jamii wenyeji kwenye oparesheni hiyo.

Soma pia : Wahudumu wa malori wamulikwa juu ya utumikishwaji wa watoto Nakuru

Wakazi waikosoa serikali

Picha: Wakio Mbogho/DW

Mwakilishi wa Kenya kwenye bunge la jumuiya ya Afrika Mashariki Florence Jematia ametuhumiwa kuchochea vita katika eneo la Baringo Kusini na amekuwa korokoni tangu alipokamatwa jumatano wiki hii. Jematia ameachiliwa hii leo kwa dhamana ya shilingi milioni moja, akiagizwa kutozuru Baringo Kusini au kuhudhuria mikutano ya kisiasa anaposubiri kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya matamshi ya chuki.

Baadhi ya viongozi wa maeneo haya wameikosoa serikali kwa kile wanasema ni kutowashughulikia wananchi wa sehemu hizo ipasavyo.

Soma pia : Nakuru yapandishwa hadhi na kuwa jiji, lakini nini maana yake?

Waziri wa usalama wa ndani Fred Matiangi amekariri kuwa wako macho kuwakamata na kuwashtaki viongozi wanaofadhili mashambulizi hayo, na pia viongozi wa kitamaduni wanawafanyia vijana matambiko na kuwaingiza kwenye kwenye itikadi hizo potofu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW