Kenya yatenga shilingi bilioni 2 kupambana na njaa
23 Septemba 2021Kitisho cha njaa na utapiamlo sugu kinawaandama watoto na kina mama wajawazito katika kaunti za kaskazini na pwani ya taifa hilo la Afrika Mashariki.
Akizindua rasmi mpango na kuwakabidhi chakula cha msaada cha mifugo, Waziri wa masuala ya Ugatuzi Eugene Wamalwa aliweka bayana kuwa serikali imetenga shilingi bilioni 2 kupambana na dhoruba za ukame.
Hela hizo zimetoka baada ya rais Uhuru Kenyatta kutangaza janga la kitaifa la ukame na kuamuru hatua kuchukuliwa wiki mbili zilizopita.
Matrela 9 na malori 6 yamesheheni magunia alfu 32 ya chakula cha wanyama kuwapa ahueni wafugaji wa kuhamahama kwenye maeneo ya kaskazini mwa Kenya.
Malori hayo yanatazamiwa kuwasili Mandera, Wajir, Garissa na Isiolo kuanzia kesho.
Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa alisisitiza pia kuwa wanaupiga jeki mpango wa kugawa hela kupambana na njaa pamoja na chakula cha msaada kwa binadamu na wanyama.
Kupitia shirika la Umoja wa mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, serikali imepokea shilingi milioni 308 zitakazotumika kununua chakula cha wanyama, dozi za chanjo,kugawa hela za matumizi na kuchimba visima. Carla Mucavi ni mkurugenzi wa FAO nchini Kenya.
Ili kuimarisha operesheni hiyo wawakilishi wa serikali na mamlaka ya kudhibiti ukame nchini Kenya watakwenye nyumba hadi nyumba kuhakikisha kuwa waathiriwa wamepokea hela na msaada huo.
Azma ya serikali ni kusambaza chakula cha mifugo cha msaada hadi kaunti za pwani ambazo ziko hatarini.Juhudi hizo zinaungwa mkono na uongozi wa kaunti.
kwa mujibu wa takwimu za mamlaka ya kudhibiti ukame nchini Kenya,tathmini ya Agosti mwaka huu imebaini kuwa watoto 652,960 na kina mama wajawazito au wanaonyonyesha wanahitaji msaada kwasababu ya utapia mlo sugu.
Kiasi ya watoto alfu 50 kati ya wote hao wako katika kaunti ya Turkana.