1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yafunga shule baada ya kisa cha tatu cha corona

Josephat Charo
15 Machi 2020

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amethibitisha kisa cha tatu cha maambukizi ya virusi vya corona na kuamuru shule zote zifungwe.

Kenia Coronavirus  Uhuru Kenyatta Meeting
Picha: PSCU

Kwa mara ya kwanza Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amekivunja kimya chake kuhusu ugonjwa wa Corona. Rais Uhuru ameamuru shule zote za kushinda kutwa nzima kufungwa kuanzia siku ya Jumatatu. Shule za mabweni zimepewa muda hadi Jumatano kuhakikisha wanafunzi wote wanarejea nyumbani kwao kwa sababu ya homa ya Corona. Vyuo vikuu na vile vya amali vimepewa muda hadi Ijumaa kuwapa nafasi wanafunzi wote kurejea kwao.

Rais Uhuru kadhalika amethibitisha kuwa watu wengine wawili wameambukizwa virusi vya corona nchini Kenya. Mmoja alitangamana na aliyeambukizwa akiwa kwenye karantini hospitalini Kenyatta. Wahudumu wa afya wanaendelea kuwatazama walioambukizwa na pia kuwatibu.

Kutokana na hali hii, wasafiri wanaotokea nchi za kigeni zilizoathiriwa na homa hiyo ya Corona wamepigwa marufuku kuingia ndani ya mipaka ya Kenya. Watakaoruhusiwa kuingia nchini ni wakenya na wageni walio na vibali rasmi. Wakenya wote watakaorejea nyumbani katika muda wa saa 48 zijazo watalazimika kujiweka kwenye karantini na kusalia ndani.

Wakenya waliotangamana na mgonjwa wa corona wawekwa karantini

Kufikia sasa watu 22 wamewekwa katika karantini ambao wanaaminika kutangamana na mkenya wa kwanza aliyegunduliwa kuambukizwa virusi vya COVID 19 mwishoni mwa wiki iliyopita. Wagonjwa hao wanapewa matibabu kwenye hospitali za Mbagathi na Kenyatta zilizo na vituo maalum vya kuwahifadhi. Ili kupata maelezo ya ziada, Wakenya wanaweza kupiga simu kwa nambari 719 au kupitia ujumbe mfupi kwa kutumia *719# kwa usaidizi wa kiafya.

Rais Uhuru Kenyatta akikutana na baraza la kitaifa la usalama kujadili suala la coronaPicha: PSCU

Kulingana na mratibu mkuu kwenye Wizara ya Afya Mercy Mwangangi, vituo viwili vya kutoa ushauri nasaha vimeandaliwa kwenye hospitali za Kenyatta na Mbagathi mahsusi kwa walioko kwenye karantini pamoja na familia zao. Kwa upande mwengine watakaopatikana wakisambaza video za kuogofya na zisizokuwa na maelezo sahihi watachukuliwa hatua za kisheria baada ya uchunguzi kukamilishwa na idara ya upelelezi.

Vilabu vyafungwa Mombasa

Wakati huo huo serikali ya kaunti ya Mombasa imepiga marufuku vilabu vyote vya densi vya usiku kuendesha operesheni zao kwa siku 30 zijazo. Baadhi wameipinga na kuikosoa hatua hiyo kwa madai kuwa hawakushirikishwa kutoa maoni yao. Marufuku hiyo ilitangazwa siku ya Jumamosi nagavana Ali Hassan Joho ili kuzuwia uwezekano wa maambukizi ya virusi vya COVID 19.

Hata hivyo vilabu vya pombe vya kawaida vimeruhusiwa kuendelea na operesheni zao hadi saa tano usiku. Wanaotembelea wagonjwa hospitalini wametahadharishwa kuwa ni watu wawili pekee wa familia watakaoruhusiwa kuwaona waliolazwa. Kwa sasa makanisa, miskiti na taasisi za kidini zinashauriwa kuhakikisha washirika wao wanapata dawa maalum ya kuosha mikono kadhalika maji na sabuni. Wasafiri kwenye magari ya umma wanashauriwa pia kuepuka msongamano na kutangamana.

(Thelma Mwadzaya)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW