Kenya yaunga mkono mpango wa Morocco kuhusu Sahara Magharibi
27 Mei 2025
Mzozo huo ambao umedumu kwa muda mrefu kuanzia mwaka 1975, unaihusu Morocco, ambayo inalichukulia eneo hilo la Sahara Magharibi kama himaya yake, dhidi ya chama cha Polisario kinachoungwa mkono na Algeria, na ambacho kinapigania ukombozi wa Sahara Magharibi.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mazungumzo kati ya mawaziri wa masuala ya kigeni wa nchi hizo mbili mjini Rabat, Kenya ilisema inautazama mpango wa Morocco kama suluhisho pekee la kuaminika na la kweli na mbinu pekee endelevu ya kuutatua mvutano huo. Musalia Mudavadi, Waziri wa masuala ya kigeni wa Kenya anaeleza.
''Suala hilo ambalo linajadiliwa kupitia michakato ya kidiplomasia iliyoanzishwa na Mfalme Mohammed wa Sita, ni jambo ambalo kwa hakika linahitaji umakini mwingi, na linahitaji uungwaji mkono mwingi ili tupate azimio la amani", alisema Mudavadi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco Nasser Bourita aliwaambia waandishi habari kwamba msimamo huo wa Kenya kuhusu Sahara Magharibi, ambao aliuita "lengo la pamoja linaloyaunganisha mataifa", ulisaidia kuongeza msukumo mpya katika uhusiano wa nchi hizo mbili.
Hatma ya uhusiano na Algeria ?
Baada ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia baina ya Kenya na Morocco, Kenya pia ilifungua ubalozi mjini Rabat siku ya Jumatatu, uzinduzi uliohudhuriwa na Mudavadi ambaye ameitaja hatua hiyo kama ishara ya kiwango kipya cha ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili. Jessica Gakinya ndiye balozi wa Kenya nchini Morocco.
Wachambuzi wanaitaja hatua hii kama ushindi kwa Morocco hasa kwa vile sasa Kenya imeachana na msimamo wake wa Sahara Magharibi. Wanasema mwaka 2017 Morocco ilichukua jukumu muhimu katika kuhakikisha kushindwa kwa mwanadiplomasia Amina Mohammed wa Kenya ambaye alikuwa akiwania kiti cha Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, baada ya mkutano wake na Brahim Ghali, kiongozi wa sasa wa Sahara Magharibi katika kambi ya Tindouf. Wakati huo Kenya ilikuwa inaiunga mkono Algeria.
Kufuatia ziara yake nchini Morocco, Waziri Mudavadi amesema Kenya sasa inatazamia kusafirisha chai zaidi, kahawa na mazao mengi ya shambani nchini Morocco ili kusawazisha biashara yake. Kenya na Morocco zimetia saini mikataba mitano katika sekta za kilimo, ujenzi wa nyumba za bei nafuu, elimu, biashara, huduma za kigeni, na masuala ya vijana.