1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yawaachilia huru wafungwa 14,000

Shisia Wasilwa23 Aprili 2021

Serikali nchini Kenya imewaachilia huru wafungwa 14000 kama sehemu ya mpango wa kupunguza msongamano katika magereza, wakati ugonjwa wa Covid-19 unapoongezeka.

Kenia Symbolbild Gefängnis
Picha: picture-alliance/dpa/D. Kurokawa

Mpaka sasa wafungwa saba na wafanyikazi saba wa magereza wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo.

Hatua hiyo inajiri wakati ambapo serikali ikisema kuwa hakuna mipango ya kuwapa chanjo ya kukabiliana na virusi vya corona wafungwa wote wa magereza.

Idara ya Mahakama pamoja na Wizara ya Afya, zinashirikiana kwenye mpango huo wa kuwaachia wafungwa huru, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka.

Wafungwa ambao wameeachiliwa ni wale waliofanya makosa madogo madogo. Idara ya Mahakama pia, inaweka mipango ya kuwaachia wafungwa ambao wanakaribia kukamilisha muda wa vifungo vyao.

Soma zaidi: Kenya kutuma wanajeshi DRC kupambana na ugaidi

Hata hivyo wafungwa hao walioachiwa wataendelea kufanya kazi katika jamii zao kwa kipindi walichostahili kuhudumu, kama njia ya kuwapatanisha na jamii. Alice Wahome ni wakili na pia mbunge wa Kandara. "Magereza yamejaa, wakati mwingi hakuna chakula. Kamishna Mkuu wa magereza anahudumu kwenye mazingira magumu.”

Kwa sasa taifa la Kenya lina zaidi ya wafungwa 40000 kinyume na idadi ya wafungwa 30000 wanaohitajika. Akizungumza alipozuru gereza la Naivasha, Katibu Mkuu wa Hudumu za Kurekebisha tabia Zeinab Hussein, aliafiki kuwa msongomano wa wafungwa magerezani ni changamoto kubwa, lakini akawa mwepesi wa kusema kuwa suala hilo linatafutiwa ufumbuzi.

Ameongeza kusema kuwa Jaji mpya ameteuliwa kushughulikia suala la kuwaachia wafungwa, hatua ambayo itaharakisha mchakato huo. Wafanyikazi 8000 wa Magereza wamepata chanjo ya AstroZeneca ya kukabiliana na virusi vya corona, hata hivyo hakuna hata mfungwa mmoja ambaye amechanjwa. Paul Korir ni mkuu wa polisi katika eneo la Mumias anafafanua, "Tumekuwa na changamoto ya kuwapima wafungwa na watuhumiwa virusi vya covid-19. Hatukupata vifaa kutoka kwa wizara ya afya.”

Huenda hatua hiyo ikazidisha usaambaji wa virusi hivyo, hata hivyo Kamishna Mkuu wa Magereza Wycliffe Ogalo ametoa hakikisho kuwa magereza yote nchini yameweka mikakati ya kukabiliana na virusi hivyo kama vile kuweka sabuni, maji kwenye vituo vya kuingia na kuondoka magerezani na pia kuvalia barakoa. 

Wakati huo huo, Naibu Inspekta Mkuu wa polisi Edward Mbugua  amewaagiza maafisa wote wa polisi wanaotekeleza maagizo ya kuzingatia vizuizi vya kukabiliana na virusi vya corona kuwapa dhamana watu wanaokiuka sheria hizo ili wasifikishwe rumande.

Wafungwa wa makosa madogo madogo pia hawafai kuzuiliwa kwa zaidi ya saa 24. Kesi zinazopewa uzito kwa sasa ni pamoja na mauaji, ugaidi, wizi wa mabavu na ulanguzi wa dawa za kulevya. 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW